Jeshi la Magereza lapunguza idadi ya wageni wanaotembelea wafungwa kujihami dhidi ya Corona

Na Doreen Aloyce,Dodoma

Ili kukabiliana na maambukizi virusi vya korona vinavyosababisha ugonjwa wa UVIKO-19, Jeshi la Magereza mkoani hapa limepunguza idadi ya wageni wanaotakiwa kuwatembelea Wafungwa na Mahabusu hadi kufikia wawili kwa wiki.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, SACP Justine Kaziulaya katika makao makuu ya Jeshi Msalato Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na DIRAMAKINI Blog.

SACP Kaziulaya amesema, Jeshi la Magereza limepokea na kufanyia kazi muongozo wa namba moja uliotolewa na Kamati ya Kitaifa iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu, kutafuta namna sahihi ya kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti mikusanyiko isiyo ya lazima.

"Sisi Magereza tumepewa dhamana ya kuwapokea na kuwahifadhi wafungwa na mahabusu, kwahiyo lazima tuchukue tahadhari sana, kwa sababu kila siku tunapokea watu wapya, hivyo tunafuata miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Afya.

"Na tunaendelea kutoa elimu kwa maafisa na Askari pamoja na Wafungwa na Mahabusu namna ya kujikinga na hata Kutoa elimu juu ya chanjo,"  ameongeza SACP Kaziulaya.

Akizitaja hatua zinazoendelea kuchukuliwa mpaka sasa ni pamoja na kuweka vifaa vya kupimia joto la mwili 'Thermoscanners' kwa ajili ya kuwapima wote wanaoingia katika maeneo ya Magereza.

Pia ameongeza hatua nyingine ni kupunguza idadi ya wageni wanaokuja kuwatembelea Wafungwa na Mahabusu hadi kufikia wawili kwa wiki, kupunguza muda wa mazungumzo kati ya mfungwa na ndugu aliyekuja kumtembelea hadi kufikia dakika tano, pamoja na kuendesha kesi kwa njia ya mtandao.

Vilevile Kaziulaya amesema, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya uwepo wa wagonjwa wa Corona katika Magereza yote hapa nchini.

"Tunawajulisha kuwa Jeshi la Magereza litaendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga kama inavyoelekezwa, na kubwa zaidi ni kwamba mpaka Sasa hakuna taarifa yoyote ya uwepo wa Mgonjwa wa Corona Katika Magereza yetu hapa nchini,"aliongeza Kaziulaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news