NENDENI MKATATUE KERO ZA ARDHI KWA WANANCHI-NAIBU WAZIRI MABULA

Na Munir Shemweta, KONGWA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kutoka ofisini na kwenda kusikiliza kero za ardhi katika halmashauri zao ili kuondoa migogoro ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma alipowasili kwa ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana.

Dkt.Mabula alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kibaigwa katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma akiwa katika ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi kwenye mikoa ya Morogoro na Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema, kero nyingi za ardhi katika halmashauri nchini hazihitaji Waziri ama ngazi ya Wizara kwenda kuzitafutia ufumbuzi bali zinaweza kutatuliwa na maafisa ardhi waliopo kwenye halmashauri husika.

‘’Ninachotaka kuona mnatoka kwenda kufanya vikao vya kusikiliza changamoto za ardhi katika halmashauri zenu na hata kama hakuna kero katoeni elimu watu wajue, maana wananchi wanauza ardhi hovyo na hawajui hata mipango ya matumizi ya ardhi na pia hawajui faida za kupimiwa na kumilikishwa,"amesema Dkt. Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akiungumza na wananchi wa Mji mdogo wa Kibaigwa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana. Wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa Remidius Mwema.

Alimtaka Kamishna wa Ardhi Msaidzi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge kuhakikisha anasimamia watendaji wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wake kutoa elimu ya masuala ya ardhi badala ya kusubiri wananchi kufika ofisi za ardhi kuwasilisha malalamiko.

Wananchi wa Mji Mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa waliwasilisha malalamiko yao kwa Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula na kumtaka awasaidie kupata ufumbuzi wa changamoto zao baada ya kukwama kutatuliwa kwa muda mrefu na Maafisa Ardhi katika halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Mkazi wa Kibaigwa wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma akiwasilisha kero yake ya ardhi kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana.

Malalamiko mengi yaliyowasilishwa mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi katika mkutano huo yalikuwa ni kuhusiana na kudhulumiwa maeneo kwa baadhi ya wananchi, udaiji fidia, uingizaji mifugo kwenye mashamba ya wakulima, ucheleweshaji kesi za ardhi katika mabaraza ya ardhi pamoja na kutokamalika kwa zoezi la urasimishaji kwa baadhi ya maeneo.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge alisema kupitia mkutano huo wa hadhara wa Naibu Waziri wa Ardhi kuwa, kutokana na kukua kwa mji wa Kibwaigwa ofisi yake ina mpango wa kuandaa Mpango Kabambe wa Mji wa Kibaigwa.

Sambamba na hilo aliongeza kuwa, kutokana na kuibuka kwa kero nyingi za ardhi katika mji huo sasa ofisi yake itaakwenda katika mji huo na timu ya wataalamu wa sekta ya ardhi na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ili kusikiliza migogoro ya ardhi na kuipatia ufumbuzi.
Sehemu ya wananchi wa Mji mdogo wa Kibaigwa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma waliojitokeza katika mkutano wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana.

‘’Sisi tutakuja kama mkoa kusikiliza migogoro mingine midogomidogo pamoja na kutoa hati na tutakuja na maafisa ardhi, wapima ardhi na msajili wa hati pamoja na msajili msaidzii wa mabaraz ya ardhi maana masuala mengi yaliyoelezwa yanahusu mabaraza walau ajaribu kuelimisha wananchikutoa,"amesema Kabonge. TAZAMA VIDEO HAPA CHINI.



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news