Serikali yatoa onyo kali watakaotoza fedha chanjo ya Corona

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa angalizo kwa wasimamizi wa chanjo kutolipisha watu fedha kwani chanjo hizo ni bure huku ikihimiza kuzingatiwa kwa weledi.Katibu Mkuu (Afya), Prof. Abel Makubi ameyasema hayo leo wakati wa usambazaji wa chanjo hizo kwenda mikoa mbalimbali nchini tukio lililofanyika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Kurasini mkoani Dar es Salaam.

Prof. Makubi amesema, utoaji wa chanjo hizo kwenye hospitali za umma na binafsi utatolewa bila kulipisha gharama za chanjo.

“Naelekeza kwa huu mgao wa Covax Facility ni marufuku hospitali za umma au binafsi kulipisha eananchi gharama yoyote katika zoezi hili la chanjo na lifanyike kwa uadilifu na kwa haki kwa walengwa wa sasa,”amesema Prof. Makubi.

Ameongeza kuwa, pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kufanikisha upatikanaji wa chanjo hizo na kuanza kuchanja wananchi, Wizara ya Afya inaendelea kuwashauri Wananchi kujikinga na UVIKO-19.

“Kwa kuzingatia kanuni za UVIKO 19, tunapaswa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kukaa umbali za mita moja au zaidi, kuepuka misongamano na kufanya mazoezi,"amesema.

Pia amesema, ugawaji wa chanjo umezingatia taarifa ya visa vya wagonjwa waliohisiwa kuwa na UVIKO-19, idadi ya walengwa kwa kundi la kipaumbele pamoja na idadi ya chanjo zilizopatikana kwa sasa.

Wakati huo huo Serikali kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara Kuu ya Taifa na vyombo vingine vyote vimehakiki na kujiridhisha usalama na ubora wa chanjo za Janssen kutoka Kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani.

Prof. Makubi amebainisha kuwa, kutokana na Mwongozo wa Chanjo wa Taifa dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO, Shirika la Afya Duniani (WHO), maelekezo ya Covax Facility na upungufu wa uzalishaji wa chanjo toka viwandani, chanjo hizo kwa sasa zinatolewa kwa kufuata vipaumbele vya makundi yenye uhitaji mkubwa.

“Makundi ambayo yataanza chanjo ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya, watu wazima umri wa miaka 50 na kuendelea na watu wenye magonjwa. Kama ambavyo Serikali imekuwa ikieleza, uchanjaji kwa makundi yote nchini ni wa hiari au huru kwa kila mwananchi. Kwa kuwa chanjo zilizopokelewa kwa sasa hazitoshelezi walengwa wa makundi yote nchini, makundi mengine yatapata chanjo katika awamu inayofuata, mara zitakapowasili,”amesema Prof. Makubi.

Hadi sasa Serikali inategemea kutoa chanjo kwa makundi yanayolengwa kuanzia tarehe 3 Agosti 2021, siku ya Jumanne, katika vituo 550 vya kutolea huduma katika mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo orodha ya vituo hivyo inapatikana pia katika tovuti ya wizara ya www.moh.go.tz.

Wananchi wote walengwa, wanaotaka kuchanjwa kwa hiari yao, huku wakitakiwa; kujihakiki kama wapo ndani ya makundi matatu ya walengwa kwa sasa.

“Mlengwa atakayepata chanjo anapaswa kuandaa kitambulisho cha kazi, NIDA, Leseni ya Udereva, Mpiga kura, Pasi ya Kusafiria au kitambulisho chochote kinachotambulika kisheria.Kufanya ‘booking’ ya siku ya kuchanjwa kwa kutumia mtandao ndani ya simu/Computer (online) yako kupitia https://chanjocovid.moh.go.tz au kwa kwenda moja kwa moja kwenye kituo na kujisajili kuanzia Jumatatu tarehe 2 Agosti
2021,"amesema Prof. Makubi.

Post a Comment

0 Comments