Aliyekuwa DED Temeke,Lusubilo Mwakabibi, Edward Haule wafikishwa mahakamani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Lusubilo Mwakabibi ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke na mratibu wa mradi wa uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Edward Haule wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka wakati wa utumishi wao.
Mwakabibi na mwenzake wamefikishwa mahakamani hapo leo Agosti 20, 2021 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na jopo la mawakili watatu waandamizi wa Serikali.

Mawakili hao wameongozwa na Mshanga Mkunde mbele ye hakimu mkazi mwandamizi, Evodia Kyaruzi wa Mahakama hiyo iliyopo jijini Ilala mkoani Dar es Salaam.

Wakili Martin mbele ye hakimu mkazi mwandamizi, Evodia Kyaruzi amedai katika shtaka la kwanza ni matumizi mabaya ya ofisi, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Machi 2020 na Machi 2021 katika Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Inadaiwa siku hiyo, Mwakabibi na Haule wakiwa waajiriwa wa Manispaa hiyo, katika utekelezaji wa ardhi walielekeza ujenzi wa stendi ya mabasi eneo la Buza katika kiwanja kinachomilikiwa na Dayosisi ya Kanisa la Anglikana bila kuwa na ruhusa.

Aidha, shitaka la pili ni matumizi mabaya ya madaraka, tukio wanaodaiwa kulitenda Machi 2020 na Machi 2021 katika eneo hilo, washtakiwa kwa makusudi wanadaiwa walitumia madaraka yao vibaya kinyume na kifungu cha 3(1) Cha Sheria ya Ardhi na kifungu cha 3,4,5,7 na 11 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 2019.

Wakili Mshanga amedai upelelezi haujakamilika na hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakati huo huo upande wao utetezi ukiongozwa na Jeremiah Mtobesya na Benedict Ishabakaki uliiomba mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa hao kwa kuwa, mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao hayajataja kiasi cha fedha katika hati ya mashtaka.

Hakimu Kyaruzi baada ya kusikiliza maombi hayo, alitoa masharti ya dhamana dhidi ya washtakiwa, ambapo amesema kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Shilingi milioni 10.

Pia washtakiwa wanatakiwa kuwasilisha fedha taslimu milioni kumi au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo, kutoruhusiwa kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kuwa na kibali cha Mahakama, pamoja na kuwasilisha hati za kusafiria.

Aidha,Hakimu Kyaruzi baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 2, 2021 na washtakiwa wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana.


Waziri Mkuu

Hayo yanajiri baada ya hivi karibuni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya uchunguzi ili kubaini kwanini uongozi wa Manispaa ya Temeke ulianza kulipa mkopo wa shilingi Billioni 19 miezi miwili baada ya kupokea ilihali mkataba ulionyesha wana-'grace period ya miezi sita.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za Kijichi-Mwanamtoti na Kijichi-Toangoma wilayani Temeke na kituo cha Mabasi kilichopo Buza ambapo amekiri kutoridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo.

"Tunatakiwa tujue hili jengo mkurugenzi gani alikopa bil.19 na kwa ajili ya nini, mkataba ulisema wana grace period ya miezi 6 na kuendelea wao wamelipa mwezi wa pili hela walitoa wapi kabla hawajazitumia zile za mwanzo kwanini waliharakisha kuzilipa na je ziliingia benki, tafuta mweka hazina aliyehusika kwenye kukopa hiyo fedha arudushiwe Temeke kuja kujibu hawezi kuhamishwa huku kuna matatizo," amesema Mhe. Majaliwa.

Pia Mhe. Majaliwa ameshangazwa na na kitendo kilichofanywa na manispaa hiyo ambayo iliwahamisha kwa haraka wale watumishi wenye shida wote huku akitoa agizo la Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kukaa pembeni kwa kile kinachodaiwa kutokuwa na majibu yanayoridhisha.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya ahakikishe anasimamia na anazingatia maslahi ya wana-Temeke katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Wananchi Serikali yenu iko macho kweli kweli na hakuna sarafu itakayotoweka tunailinda na Mawaziri tupo kwa ajili hiyo na tuna maelekezo thabiti ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na watumishi wa umma tupo hapa kuwahudumia wananchi,” amesema Mhe. Majaliwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news