Mbunge Askofu Gwajima atiwa hatiani bungeni

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imetoa ripoti yake leo Agosti 31,2021 Bungeni jijini Dodoma kuhusu shauri la Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima baada ya kumaliza kumuhoji kwa tuhuma za kuzungumza uongo na kulishushia Bunge hadhi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maadili, Emmanuel Mwakasaka amewasilisha ripoti hiyo mbele ya Bunge.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo wakati akisoma taarifa yake amesema shahidi ambaye ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima alikiri kauli zote ni zake asilmiia 100 huku akisitiza yalikuwa ni mahubiri.

"Niliyasema nikiwa kanisani (Ufufuo na Uzima) na ninayasema kama Askofu, kosa kubwa ni kujaribu kuyakosoa mahubiri, huwezi ku-question mahubiri, Kamati ilijiridhisha kuwa mahubiri yanayotolewa yanapaswa kuzingatia sheria za nchi,hivyo kauli zinazotolewa haziwezi kuwa na kinga ya kuhojiwa.

“Gwajima ni Mbunge na Kiongozi kwa hiyo anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa, tuhuma za kuchonganisha Mhimili wa Bunge na Serikali au Serikali na wananchi zinajidhihirisha wazi kwenye kauli za Askofu Gwajima,"amefafanua Mwenyekiti huyo.

Ameongeza kuwa “Gwajima alishindwa kuthibitisha kauli zake na hana kielelezo chochote kama alivyowaaminisha wananchi, suala la viongozi kupewa rushwa hakutoa ushahidi wowote, kamati imemtia hatiani Askofu Gwajima.

“Kuhusu adhabu ya utovu wa nidhamu uliokithiri wa Askofu Gwajima ni kuwa kanuni zinataka asihudhurie mfululizo mikutano miwili au isiyopungua mitatu, Kamati ilishangazwa na vitendo alivyovifanya mbele yake na iliona ni dharau.

“Askofu Gwajima hakukiri wala kujutia makosa yake, alionyesha dharau hivyo Kamati imemtia hatiani, Bunge linaazimia kuwa apewe adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili mfululizo ya Bunge baada ya kupitisha azimio hili,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news