SHEKILINDI KUNUNUA DAWA ZA 500,000/- ZAHANATI YA KWEMASHAI

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi ameahidi kutoa sh. 500,000 kwa ajili ya kununua dawa Bohari ya Dawa nchini (MSD) ili zipelekwe kwenye Zahanati ya Kata ya Kwemashai.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi "Bosnia" (katikati) akikagua ujenzi wa Ofisi ya Serikali Kijiji cha Ngulu, Kata ya Kwemashai. Ameahidi kutoa bati za kuezeka ofisi hiyo. (Picha na Yusuph Mussa).

Aliyasema hayo hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ngulu. Ni baada ya wananchi kulalamika kuwa, pamoja na kuwepo zahanati hiyo dawa hazitoshelezi, ambapo inawafanya kusafiri umbali mrefu kufuata dawa Lushoto mjini.

"Naahidi kuleta dawa za sh. 500,000 kwenye Zahanati ya Kwemashai ili wananchi wangu msiweze kupata shida ya dawa. Na mimi kama Mbunge wenu, najua mgawo wa dawa ni mdogo kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu, hivyo lazima nifanye jitihada za kupata dawa, hata kwa pesa zangu za mfukoni," alisema Shekilindi.

Shekilindi alisema, anajua umuhimu wa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya afya, hivyo ataunga juhudi za wananchi kuona Zahanati ya Kijiji cha Ngulu, Kata ya Kwemashai nayo inakamilika. Lakini pia atafanya jitihada kuona Zahanati ya Kwemashai inaongezewa jengo moja ili kutoa huduma kwa urahisi kutokana na idadi kubwa ya wananchi.

Pia ameahidi kuwanunulia betrii ya Solar kwenye Zahanati ya Kwemashai, kwani kabla ya hapo alishanunua Solar na betrii yake, lakini wananchi wamesema kwa sasa betrii hiyo ni mbovu. Pia amesema Serikali itakamilisha maabara Shule ya Sekondari Kwemashai, atatoa bati kwa ajili ya darasa Shule ya Msingi Kilangwi, na kutoa bati na saruji kwa ajili ya umaliziaji wa Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Ngulu.

"Hatuna wazungu ndugu zangu, sisi wenyewe ndiyo tunatakiwa kuchangia maendeleo yetu. Hivyo kukipigwa gunda (msalagambo), basi tujitokeze kuweza kuchangia shughuli za maendeleo. Ni kweli, Serikali itafanya ukarabati wa shule zote kongwe za msingi na sekondari, lakini tunatakiwa na sisi tuanze," alisema Shekilindi ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Kilangwi, Kata ya Kwemashai.

Katibu wa CCM Tawi la Ngulu, Kata ya Kwemashai Awadhi Salum alisema Shule ya Msingi Chumbageni iliyopo Kijiji cha Ngulu majengo yake yamechoka, huku baadhi ya madarasa yakiwa hayana sakafu, hivyo kila siku watoto wanachafuka, hivyo kila siku wazazi wananunua sabuni.

"Shule ya Msingi Ngulu tumechoka kununua sabuni kila siku kwa ajili ya kufua sare za watoto wetu. Vyumba vya madarasa vimechakaa, watoto wanasoma kwenye vyumba havina sakafu, hivyo kuwa hatarini kupata funza. Na hapa niseme, hili suala sio la kumlaumu mwalimu kama mtoto hatafaulu, kwani hata kama mtoto ana akili kiasi gani, hawezi kufaulu kwenye mazingira haya," alisema Salum.

Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Kwemashai Ramadhan Sabuni alisema baadhi ya wauguzi wa Zahanati ya Kwemashai pamoja na walimu wa shule za msingi na sekondari kwenye kata hiyo hawaishi hapo, bali wanakwenda kazini na baadae kurudi Lushoto mjini, na hiyo ni kutokana na uhaba wa nyumba kwa watumishi hao. Hivyo wanaomba Serikali ya Awamu ya Sita kuweza kujenga nyumba za watumishi hao.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chumbageni Awadhi Bushiri alisema moja ya sababu ya shule hiyo vyumba vya madarasa kuchakaa ama kushindwa kuongeza vyumba vingine vya madarsa inatokana na dhana potofu kuwa elimu inayotolewa nchini kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne ni bure, wakati hiyo sio kweli, bali elimu inatolewa bila malipo.

"Elimu sio bure, bali bila malipo. Kutokana na dhana hiyo wazazi wanadhani hawatakiwi kuulizwa chochote kuhusu maendeleo ya watoto wao, kuwa wanatakiwa kuchangia kukarabati madarasa mabovu au kujenga vyumba vingine vya madarasa, wakati kuna wenzetu wengine wanachangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili watoto wao wasikae kwenye mavumbi,"alisema Bushiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news