Waziri Chilo avitaka vyombo vya ulinzi vitoe elimu kuhusu Corona

Na Abubakari Akida, MOHA

VYOMBO vya Ulinzi na Usalama nchini vimetakiwa kutokujiweka kando na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Virusi vya Korona katika kipindi hiki ambacho nchi inapitia katika vita ya wimbi la tatu la ugonjwa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Sophia Jongo akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo (kushoto) wakati wa ziara ya kikazi iliyofanyika mkoani Tabora.(Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).

Rai hiyo imetolewa leo mkoani Tabora na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani hapo ambapo alieleza mapambano ya ugonjwa huo ni suala linalotakiwa kushirikisha wizara zote zikiongozwa na wizara husika ya afya.

“Vyombo vya Ulinzi na Usalama mnayo nafasi kubwa katika mapambano dhidi ya maradhi ya Virusi vya Korona,mna mahabusu wako vituo vya polisi sehemu mbalimbali nchini,mna mahabusu wako katika magereza,tuna askari wetu wa usalama barabarani basi ili mradi kila sehemu mnahusiana na jamii moja kwa moja hivyo natoa wito kwa vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama nchi nzima mhakikishe katika kazi zenu za kila siku mtoe elimu ya kujikinga na maradhi hayo,”amesema Naibu Waziri Chilo.

“Lakini pia tahadhari hiyo ya kujikinga na maradhi hayo pia iende kugusa shughuli zenu za kila siku ikiwemo na nyie wenyewe kujikinga ili tusipoteze nguvu kazi ya taifa,Rais Samia Suluhu Hassani anawategemeeni sana katika kulinda amani na utulivu wan chi hii,”ameongeza Naibu Waziri Chilo.

Awali akisoma taarifa ya hali ya ulinzi na usalama ya mkoa huo,Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora,Kamishna Msaidizi wa Polisi Sophia Jongo alisema, kumekuwepo na kupungua kwa matukio ya uhalifu katika mkoa huo huku jeshi la polisi likiendelea na operesheni mbalimbali katika kuhakikisha matendo ya uhalifu yanapungua.

“Mheshimiwa Naibu Waziri katika mkoa wetu kulikuwepo na matukio ya kihalifu ikiwemo mauaji,Watoto watukutu kujikusanya makundi na kufanya uhalifu katika sehemu mbalimbali ikiwemo uporaji lakini sasa hivi tumedhibiti hiyo hali na sasa mkoa uko salama ama kwa upande wa mauaji tulikua tunashuhudia mauaji ya watu watatu mpaka watano kwa wiki lakini sasa hivi matukio hayo yameisha kabisa huku jeshi likiendelea kuimarisha ulinzi kupitia doria tulizonazo,” amesema ACP Sophia Jongo.

Naibu Waziri yuko mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ambapo anatumia ziara hiyo pia kutembelea makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu yaliyopo wilayani Kaliua ambayo yanatumiwa na wakimbizi waliokimbia machafuko ya kikabila nchini Burundi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news