Mazungumzo ya Rais Samia, Kansela Merkel kwa simu yafungua fursa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 1 Septemba, 2021 amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani, Mhe.Angela Merkel Ikulu jijini Dar es Salaam leo Septemba 1,2021. (PICHA NA IKULU).

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika hatamu za Urais nchini Tanzania na kumpa pole kufuatia kifo cha Aliyekuwa Rais wa Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada zake za kupambana na UVIKO 19 na kuahidi kuunga mkono jitahada hizo kwa kutoa msaada wa chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, Mhe. Merkel amesema mwezi Oktoba mwaka huu Serikali yake itaanzisha majadiliano na Serikali ya Tanzania kuhusu maeneo ambayo Serikali ya Shirikisho la Ujerumani inaweza kusaidia kutokana na athari za UVIKO 19.

Pia, Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ambapo ameahidi kuwashawishi wafanyabiashara wa Ujerumani na watalii kutembelea na kuwekeza nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Merkel kwa ushirikiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Merkel kwa kumaliza kipindi chake cha uongozi akiwa ni kiongozi wa kisiasa mwanamke aliyeongoza muda mrefu ndani ya Chama chake cha CDU na ndani ya Jumuiya ya Ulaya.

Post a Comment

0 Comments