Rais Samia:Kipindi cha miezi sita Wawekezaji wamevunja rekodi nchini

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha miezi sita ikiwa ni kuanzia mwezi Machi hadi Agosti, 2021, idadi ya wawekezaji wanye nia ya kutaka kuweza nchini imeongezeka.

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Septemba 26, 2021 wakati akisalimiana na wananchi wa Wilaya ya Dodoma Mjini waliofika kumpokea katika eneo la Chinangali, mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Wananchi wa Wilaya ya Dodoma Mjini waliofika kumpokea katika eneo la Chinangali mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam leo Septemba 26, 2021.

Amefafanua kuwa, kuna miradi ambayo hawakujua kuwa wawekezaji wanakuja,hivyo miradi hiyo itatekelezwa kama ilani ilivyoeleza na miradi mingine ilani inaeleza wawekezaji watafutwe.

“Ilani ilitutuma tutafute wawekezaji waje kuwekeza, nami nataka kuwaambia wawekezaji tumepata wengi mno. Lakini niwaambie kwamba katika kipindi cha miezi sita kumekuwa na idadi kubwa ya wawekezaji ambao wanataka kuwekeza Tanzania. Kati ya hao tuna kiwanda cha mbolea kinachoendelea kujengwa hapa Dodoma. Nawaahidi na wengine watakuja,” amesisitiza Rais Samia.

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Geoffrey Mwambe, akiongea na vyombo vya habari juu ya juhudi zinazofanywa na ofisi hiyo, pamoja na taasisi zake katika kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji nchini, aliutaja mradi wa uwekezaji wa kimkakati wa Kampuni ya ITRACOM FERTILIZERS LIMITED unaotekelezwa katika mkoa wa Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akivalishwa vazi la kimila na wazee wa kimila wa Kabila la Kigogo wenye asili ya Dodoma wilayani Chamwino kama ishara ya ukaribisho mara baada ya kuwasili Chamwino Ikulu akitokea jijini Dar es Salaam leo Septemba 26,2021.
Mzee wa Kimila wa Kabila la Kigogo Wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Bw. Goden Wenga akimkabidhi Ngao na Mkuki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kama ishara ya ukaribisho mara baada ya kuwasili Chamwino Ikulu akitokea jijini Dar es Salaam leo Septemba 26,2021. (Picha zote na Ikulu).

Amefafanua kuwa, mradi huo, utazalisha mbolea asilia. Mradi huo una mtaji wa Dola za Marekani milioni 180 na unatarajiwa kuzalisha ajira 3000. Mradi huo utaingiza fedha za kigeni na utaongeza kipato kwa wananchi na mapato ya serikali kupitia kodi.

Mhe. Mwambe alibainisha kuwa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Agosti, 2021 jumla ya miradi 133 imesajiliwa ikilinganishwa na miradi 105 iliyosajiliwa katika kipindi hicho mwaka 2020 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 27.

Miradi iliyosajiliwa katika kipindi hicho inatarajiwa kuzalisha ajira 29,709 ikilinganishwa na ajira 8,252 zilizotarajiwa kuzalishwa katika kipindi hicho mwaka 2020. Miradi hiyo ipo katika Sekta ya Kilimo, ujenzi/majengo ya biashara, nishati, Miundombinu ya kiuchumi, Taasisi za fedha, rasilimali watu, viwanda, usafirishaji, utalii na huduma.

Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji pamoja na Taasisi zake inaendelea kuwahakikishia wawekezaji kuwa itaendelea kuratibu masuala ya uwekezaji ili kuhakikisha wanakuwa na mazingira wezeshi ya uwekezaji

Post a Comment

0 Comments