Tanzania yakipigia chapuo Kiswahili kutumika mikutano ya UNWTO

NA MWANDISHI MAALUM

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amewasilisha ajenda ya kutaka lugha ya Kiswahili ianze kutumika kama lugha ya mawasiliano na lugha ya kufundishia katika mikutano itakayokuwa ikiandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Utalii Duniani ( UNWTO).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( kushoto) akizungumza na Waziri wa Utalii wa Kenya, Mhe.Najib Balala mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kimataifa wa 64 wa Utalii Kanda ya Afrika uliomamalizika kufanyika nchini humo, Wa pili kulia ni Waziri wa Utalii nchini Cape Verde ambapo wamesema kuwa lugha ya Kiswahili iwe ni agenda ya kudumu katika mikutano hiyo ili Kiswahili kiweze kutumika kama lugha ya kufundishia na mawasiliano katika mikutano ya UNWTO.

Amesema, Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na mataifa 13 na pia ina wazungumzaji takribani milioni 150 duniani.

Kufuatia hali hiyo, Dkt.Ndumbaro alipenyeza ajenda hiyo wakati akichangia hoja za kuimarisha utalii hususan katika kuziwezesha jamii kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utalii katika mkutano wa 64 wa Kimataifa wa Kanda ya Afrika ulioandaliwa na UNWTO ambao umemalizika kufanyika katika Kisiwa cha Sal nchini Cape Verde.

Katika mkutano huo ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akiwa ameambatana na Waziri wa Utalii na Mambokale Zanzibar, Mhe.Lela Mussa Mohammed.
Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii, Zurab Pololikashvili (wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi wa Cape Verde wakiwa wamesimama wakati wakiimba wimbo wa taifa hilo katika Mkutano wa Kimataifa wa 64 wa Utalii Kanda ya Afrika uliomalizika kufanyika nchini humo, Wa pili kulia ni Waziri wa Utalii nchini Cape Verde, Mhe. Carlos Santos.

Akipenyeza ajenda hiyo ya lugha ya Kiswahili kuanza kutumika kama lugha ya kufundishia ambayo ilipokelewa, Dkt.Ndumbaro amesema, ni muda muafaka sasa kwa UNWTO kuifanya lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano kwa vile nchi 13 ambao ni wanachama wa UNWTO wanazungumza lugha hiyo.

Amesema, kwa kuwa lugha zinazotumiwa kwa sasa ni Kireno, Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili pia kitumike katika mikutano hiyo ya UNWTO kwa vile lugha hiyo imejitosheleza.

Aidha, amesema lugha ya Kiswahili ni lugha ya tatu duniani kwa ukubwa na imekuwa ikitumika kama lugha ya mawasiliano katika Umoja wa nchi za Afrika ( AU ), Jumaiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi Wanachama wa SADC.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro (katikati) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe.Samwel Shelukindo pamoja na Mawaziri kutoka nchi mbalimbali barani Afrika wakifuatilia mada mbalimbali za kukuza utalii wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa 64 wa Utalii Kanda ya Afrika kabla ya kumalizika kufanyika katika kisiwa cha SAL nchini Cape Verde.
Baadhi ya Mawaziri wa Utalii Barani Afrika pamoja na Watalaamu wa masuala ya Utalii Duniani wakifuatilia Mkutano wa Kimataifa wa 64 wa Utalii Kanda ya Afrika uliomamalizika kufanyika katika kisiwa cha SAL nchini Cape Verde.

Hivyo, Dkt.Ndumbaro alishauri kuwa kwa vile mwakani Tanzania itakuwa Mwenyeji wa mkutano huo wa 65 wa Kimataifa wadau wengi wa utalii wataelewa kama lugha ya Kiswahili itatumika kama lugha ya kufundishia baadala ya kuendelea kutumia lugha ambazo idadi ndogo ya watu ndio wanayoimudu huku akisisitiza kuwa lugha hizo zina uhusiano wa moja kwa moja na Wakoloni.

Naye Waziri wa Utalii na Mambo Kale Zanzibar, Mhe.Lela Mussa Mohamed amesema licha ya ajenda ya kiswahili kupokelewa katika mkutano huo itakuwa ni ajenda ya kudumu kwa nchi zote 13 kuisemea kila wanaposhriki katika mikutano iliyoandaliwa na UNWTO kwa lengo la kukifanya Kiswahili kiwe ni miongoni mwa lugha zitakazokuwa zikitumika katika mikutano hiyo.

''Huu ni utambulisho wetu wana Afrika Mashariki na Afrika kiujumla lazima tuhakikishe lugha ya Kiswahili inatumika katika mikutano hii ili watu wetu wajue nini kinachozungumzwa kina uhusiano wa moja kwa moja kwenye maisha yao,"alilisitiza Mhe. Lela.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( kushoto ) akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Utalii na Mambo Kale Zanzibar mara baada ya kumalizika kufanyika kwa Mkutano wa Kimataifa wa 64 wa Utalii Kanda ya Afrika katika Kisiwa cha SAL nchini Cape Verde.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kondoa mjini na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii amepongeza uthubutu huo wa Dkt.Ndumbaro wa kuipigania lugha ya Kiswahili na kusisitiza kuwa kutumika kwa lugha hiyo kitakuza utambulisho wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Kufuatia hali hiyo, aliishauri Serikali kuhakikisha kila fursa kama hizo zinapojitokeza hususan katika mikutano ya kimataifa ajenda ya lugha ya Kiswahili kutumika isiachwe pembeni.

Naye Mbunge wa Rorya, Mhe.Jafari Chege ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, amesema kupenyezwa kwa ajenda ya Kiswahili ni moja ya hatua muhimu kwa vile kama lugha ya Kiswahili kitajadiliwa na kuanza kutumika katika mafunzo ambayo yataanza kutolewa na UNWTO yatachagiza maendeleo makubwa ya utalii nchini.

Post a Comment

0 Comments