WAZIRI BITEKO ASISITIZA LESENI KWENYE MILIPUKO YA MADINI

Na Tito Mselem,WM-Geita

Waziri wa Madini, Mheshimiwa Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini kufuata Sheria, Taratibu na Miongozo inayosimamia Sekta ya Madini kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini wakiwa kwenye shughuli za uchimbaji madini katika mlipuko wa madini uliotokea Kijiji cha Nyamafulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.

Waziri Biteko ametoa maelekezo hayo alipotembelea mlipuko wa madini ya dhahabu uliotokea katika Kitongoji cha Nyambogo, Kijiji cha Nyakafuru, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita baada ya mkazi mmoja wa eneo hilo kuchimba shimo la choo na kukutana na madini ya dhahabu.

Waziri Biteko amesema,kila mahali panapochimbwa madini lazima watu wachimbe kwa utaratibu na utaratibu wenyewe ni mmoja tu umetajwa na Sheria lazima mchimbaji awe na leseni ya uchimbaji.
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akizungumza jambo na viongozi wa madini wa Mkoa wa kimadini wa Mbogwe katika mlipuko wa madini uliotokea Kijiji cha Nyamafulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.

Aidha, Waziri Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wanchimbaji wote wa nchi hii wawe wanachangamkia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini ili wanufaike na madini yaliopo nchini.

“Msidanganywe na mtu, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anataka watanzania wachangamkie fursa, Rais anataka watanzania wamilki uchumi wa madini ndiyo maana amesema maeneo yanayo kaliwa na watu bila kuendelezwa tuyafute na tuwape wachimbaji wadogo, Rais wetu anawapenda sana wachimbaji na anatamani watu watoke kwenye wimbi la umasikini,” amesema Waziri Biteko.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa kimadini wa Kahama na Mbogwe, Joseph Kumburu akisoma taarifa ya maendeleo ya madini katika mkoa wa kimadini wa Mbogwe.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto) akisoma faarifa za madini katika mkoa mpya wa madini wa Mbogwe kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe,Charles Kabeho.

Pia, Waziri Biteko amewataka wachimbaji wa madini katika eneo hilo wapendane na kuthaminiana ili wachimbe kwa amani ambapo amesema hiyo dhahabu iliyopatikana katika eneo hilo isiwafanye wagombane na badala yake wapendane na kuthaminiana.

“Mmekutana hapa kwenye shughuli ya madini, pendaneni na niwaambie Wanambongwe neema hii ameileta Mungu hapa kwenu, kuna watu wanatamani wangekuwa hata na shimo moja la dhahabu lakini Mungu hajawapa ila nyinyi hapa mkichimba mnapata dhahabu, pendaneni thaminianeni,” amesisitiza Waziri Biteko.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Charles Kabeho (kulia) katika mlipuko wa madini uliotokea Kijiji cha Nyamafulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza jambo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mlipuko wa madini uliotokea Kijiji cha Nyamafulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo katika ofisi Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Charles Kabeho.Akitoa taarifa ya Mkoa Mpya wa Kimadini wa Mbogwe.

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huo, Mhandisi Joseph Kumburu amesema, Ofisi ya Mbogwe ni moja kati ya Ofisi 28 za Tume ya madini zilizopo Tanzania Bara ambapo inasimamia wilaya ya Mbogwe, Bukombe na Nyanghwale kwa shughuli zote zinazohusiana na madini.

Aidha, Mhandisi Kumburu amasema, Ofisi Mpya ya Mbogwe ilianza kutoa huduma zake tangu Julai 01, 2021 baada ya kugawanywa kwa Ofisi ya Afasa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita.
Baadhi ya washiriki walioshiriki mkutano wa hadhara uliofanyika katika mlipuko wa madini uliotokea Kijiji cha Nyamafulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.

Mpaka kufikia Agosti 31, 2021, zaidi ya Tsh bilioni 2.6 zilikuwa zimekusanywa ambapo 843,905,420.91 zilikusanywa mwezi Julai 2021 na Tsh 1,814,400,966.47 zilikusanywa mwezi Agosti 2021.

Mhandisi Kumburu amesema kuwa, baada ya kutokea mlipuko wa madini Agosti 17, 2021, zaidi ya watu 30,000 wameshavamia eneo hilo na wameanza shughuli za uchimbaji ambapo Ofisi ya madini mpaka sasa imepokea jumla ya maombi 29 ya leseni za uchimbaji mdogo na leseni mbili za utafiti katika eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments