Bayern Munich yaichakaza Bayer Leverkusen kwa mabao 5-1 Bundesliga

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Timu ya Bayern Munich imeitandika mabao 5-1 Bayer Leverkusen kwenye mechi ya Ligi Kuu nchini Ujerumani ya Bundesliga.

Ushindi huo mkubwa waliupata Oktoba 17, 2021 katika dimba la Bay Arena ukiwa ni mchezo wa kwanza baada ya mapumziko ya mechi za Kimataifa.
Katika mtanange huo, Robert Lewandowski raia wa Poland alifunga mabao mawili, Thomas Muller, na Serge Gnabry ambaye alitundika mizinga miwili nyavuni wakati goli la kufuatia machozi kwa Leverkusen likitiwa kimiani na Patrick Schick.

Lewandowski aliwapatia waajiri wake bao la kwanza daki ya tatu na lile la pili ndani ya dakika ya 30, huku Thomas Muller ndani ya dakika ya 34 akiwapatia bao la tatu.

Aidha, Serge Gnabry ndani ya dakika ya 35 aliwaandikia waajiri wake bao la nne na dakika mbili baadaye kwa maana ya dakika ya 37 alitundika mzinga wa maana golini ambalo lilifunga mjadala katika mtanange huo.

Katika kutafuta namna ya kujinasua kutoka kwenye mafuriko hayo ya mabao, Patrik Schick ndani ya dakika ya 55 aliwapatia waajiri wake Leverkusen bao la kufuta machozi.

Hata hivyo, kwa ushindi huo unaifanya Bayern Munich kufikisha alama 19 kileleni mwa msimamo wa Bundesliga alama moja zaidi ya Borrusia Dortmund wakati Leverkusen wako nafasi ya tatu kwa alama 16 tu.

Post a Comment

0 Comments