DC Tano Mwera aagiza Polisi kumkamata Mwandishi wa habari wa ITV

NA MWANDISHI DIRAMAKINI 

Mheshimiwa Tano Mwera ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa ameagiza polisi wilayani humo kumkamata na kumuhoji mwandishi wa habari wa kituo cha ITV, Baraka Lusajo.

Ni kwa madai ya kuripoti taarifa za maafa pasipo kumuhusisha mkuu huyo wa wilaya.

Lusajo akizungumzia uamuzi huo amesema kufuatia agizo hilo amehitajika na kufika katika kituo cha polisi cha Matai ambapo amehojiwa kuhusu madai hayo kisha kuruhusiwa kuondoka.

"Ni kweli mkuu wa upelelezi wilaya alinitaka nifike kituoni ambako nilichukuliwa maelezo kuhusu kuripoti taarifa ya maafa yaliyotokea katika kijiji cha Mkowe ambapo Oktaba Mosi majira ya saa 10 jioni nyumba zipatazo 30 ziliezuliwa na nyingine kubomoka huku familia 20 zikikosa makazi kabisa,"amesema.

Amesema, yeye alifika eneo la tukio akiwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kalambo, lakini alishtushwa na taarifa kwamba mkuu wa wilaya hakutaka taarifa hiyo iripotiwe katika vyombo vya habari pasipo yeye kuhusishwa.

Aidha, Mkuu wa wilaya hiyo, Tano Mwera pasipo kukiri moja kwa moja kutoa agizo hilo alidai, "wewe unaniuliza kama nani ni mwenyekiti wa Press Club?...hili suala linakuhusu nini? Haya alichokueleza Lusajo ndio hicho hicho hawezi kusema uongo," alisema Mwera.

Katibu wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Rukwa, Sammy Kisika alikiri kuwepo kwa sintofahamu kati ya mkuu huyo wa wilaya na mwandishi wa habari, Lusajo lakini akadai suala hilo linashughulikiwa na waandishi watataarifiwa hatua zilizochukuliwa.

Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa, William Mwampaghale alisema hajapata taarifa za mwandishi huyo kuhojiwa, lakini anafuatilia ili kujua ukweli wa jambo hilo.

Tukio la wanahabari wa mkoa huo kukamatwa na polisj kwa agizo la mkuu wa wilaya si mara ya kwanza, kwani mwaka juzi mkuu wa wilaya aliyekuwepo kipindi hicho, Judith Binyura aliagiza kukamatwa kwa wanahabari watatu, Gurian Adolf (Nipashe), Sammy Kisika (Azam TV) na Mussa Mwangoka (Mwananchi).

Wanahabari hao walifika katika kijiji cha Ilimba kuhoji changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho hususani mgogoro wa ardhi kati yao wakala wa hifadhi ya misitu wilaya ya Kalambo hali iliyosababisha wao kukosa maeneo ya kufanya shughuli za kilimo, ambapo nao walihojiwa na polisi kisha kuruhusiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news