Elimu kuhusu chanjo ya UVIKO-19 yawafikia waumini kanisani

Na Dennis Gondwe, DODOMA

WAUMINI wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika jijini Dodoma wameshauriwa kujitokeza na kupata chanjo ya Uviko-19 ili kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama.
Ushauri huo ulitolewa na Mratibu wa Chanjo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Victor Kweka alipokuwa akitoa elimu na kuhamasisha waumini wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika jijini Dodoma leo.

Kweka alisema kuwa ugonjwa wa Uviko-19 upo na unaendelea kuisumbua dunia na Tanzania ikiwemo. “Napenda niwataarifu kuwa bado tunawagonjwa wa Uviko-19 katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Hivyo, sote kwa pamoja tusaidiane kuendelea kutoa elimu ili tuwe salama. Bahati nzuri chanjo zipo hapa Dodoma. Tujitokeze kuchanja ili tukabiliane na ugonjwa huu,” alisema Kweka.

Akiongelea usalama wa chanjo ya Uviko-19, alisema kuwa chanjo hiyo imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Tanzania, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) wamethibitisha ubora wa chanjo hizi kuwa ni salama kutumika nchini. “Na katika Jiji la Doodma watu kadhaa wameshachanjwa na hakuna madhara yaliyojitokeza. Hii inathibitisha kuwa chanjo ya Uviko-19 ni salama” alisema Kweka kwa kujiamini.

“Kwa kuwa tumepewa muda mfupi, niwakaribishe pale nje ya kanisa kuna timu ya wataalam kutoka Jiji la Dodoma kwa ajili ya kutoa elimu na kwa wale watakaokuwa tayari wapate chanjo. Baada ya kupata chanjo kuna vyeti vitakavyotolewa na vinatolewa hapohapo, asanteni sana Bwana Yesu asifiwe sana,” alimalizia Kweka kwa unyenyekevu.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea na utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Uviko-19 kwa kutembelea taasisi mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha na kutoa huduma ya chanjo kwa watakaohamasika ikiwa katika siku yake ya tatu.

Post a Comment

0 Comments