Kombora inavyosaidia watu wengi kuchanja chanjo ya UVIKO-19

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Matangazo kwenye kumbi za video maarufu kama Kombora ambayo yamekuwa yakitolewa kuhusu taarifa mbalimbali za elimu,hamasa na ratiba za chanjo ya UVIKO-19 imesaidia kufikisha taarifa kwa wananchi na hivyo kusaidia watu wengi kujitokeza kupata chanjo.
Spika maarufu kama kombora ambazo zinatumika kutangaza na kuhamasisha masuala ya chanjo.
Mratibu wa chanjo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Nassibu Mponda akizungumza na timu ya waandishi wa habari inayofuatilia kufanya tathmini ya hali ya mpango wa chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi alisema kuwa kombora imekuwa msaada mkubwa kuwafanya wananchi wengi kujitokeza kupata chanjo.

Mponda alisema kuwa kutokana na hilo wamekuwa wakiwatumia viongozi wa vijiji na vitongoji na watoa huduma za afya katika jamii kufika kwenye vibanda hivyo kutoa taarifa mbalimbali jambo ambalo limeongeza uelewa kwa jamii lakini kuongeza hamasa kubwa kwa wananchi kutaka kuchanja.
Afisa Afya Zahanati ya Mwandiga, Constancia Petro akimpa chanjo ya UVIKO-19 mmoja wa wananchi waliojitokeza kupata chanjo.

Akiongoea timu hiyo ya waandishi wa habari Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya Kigoma,Hamisi Saidi alisema kuwa kusogezwa karibu na wananchi kwa huduma za utoaji chanjo ya UVIKO-19 kwa njia ya kutembea (MKOBA) kumechangia ongezeko kubwa la wananchi kujitokeza na kupata chanjo hiyo.

Saidi alisema kuwa, kwa siku ambazo wanafanya matangazo na kwenda kwa wananchi zaidi ya watu 50 wamekuwa wamekuwa wakijitokeza na kupata chanjo ambapo maswali mbalimbali yamekuwa yakiulizwa na kutolewa majibu hali ambayo imekuwa ikiongeza imani ya wananchi kuhusu chanjo.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mahembe halmashauri ya wilaya Kigoma,Elius Juma alisema kuwa huduma ya mkoba imewapa nafasi kubwa jamii kusikia maelezo ya watalaam lakini pia kuwa tayari kupata chanjo kutokana na watu wengi kuona kazi kufuata huduma ya chanjo kwenye vituo vya utoaji huduma.

Alisema kuwa pamoja na huduma hiyo pia kuwatumia wazee maarufu na viongozi wa dini kwenye maeneo husika imekuwa na mchango mkubwa kurudisha imani ya wananchi kuhusu chanjo hiyo na wengi kujitokeza kusikiliza maelezo yanayotolewa na kupata chanjo.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mahembe, Jumanne Mahmoud ambaye anatoa huduma ya kombora alisema kuwa kombora imesaidia sana kuhamasisha chanjo kiasi kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakifika kwenye kibanda chake kufuata chanjo.

Hata hivyo alisema kuwa, kutokana na kutokuwepo kwa watoa huduma muda wote katika eneo hilo amekuwa akilazimika kuwaandikisha majina watu wanaofuata chanjo na baadaye kuita watoa huduma ambao huwapatia chanjo wananchi hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news