Ligi Kuu Tanzania Bara yazidi kuwa ya moto

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Saadat Mohamed dakika ya 61 aliipa Ruvu Shooting ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Mtanange huo wa Oktoba 17, 2021 ulipigwa katika dimba la Mabatini mjini Mlandizi katika Mkoa wa Pwani.

Ruvu Shooting inayofundishwa na kocha, Charles Boniface Mkwasa (Master) kwa ushindi huo inafikisha alama sita baada ya mechi tatu za mwanzo kufuatia kufungwa 1-0 na Dodoma Jiji FC jijini Dodoma na kushinda 1-0 dhidi ya Biashara United mjini Musoma.

Kwa upande wa Coastal Union, hali si njema kwani wamekamilisha mechi tatu bila ushindi kufuatia sare mbili za nyumbani 1-1 na Azam FC na 0-0 na KMC dimba la Mkwakwani huko jijini Tanga.

Wakati huo huo,Mbeya Kwanza imelazimishwa sare ya 0-0 na Dodoma Jiji Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mbeya Kwanza inafikisha alama tano baada ya mechi tatu, ikitoka kushinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini na sare nyingine ya 2-2 dhidi ya mahasimu wao wa Jiji, Mbeya City, wakati Dodoma Jiji baada ya kuichapa Ruvu 1-0 nayo ilichapwa 1-0 na Simba SC nyumbani katika dimba la Jamhuri jijini Dodoma.

Awali, katika mitanange ya Oktoba 16, 2021 timu ya Geita Gold ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika dimba la Nyankumbu mjini Geita.

Danny Lyanga alianza kuifungia Geita Gold dakika ya 47, kabla ya Boban Zirintusa kuisawazishia Mtibwa Sugar dakika ya 64 katika mchezo ambao kila timu ilipoteza mkwaju wa penalti.

Kwa upande wa dimba la Kaitaba mjini Bukoba Mkoa wa Kagera, Kagera Sugar ililazimishwa sare ya bila kufungana na Mbeya City kutoka jijini Mbeya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news