Miaka 20 ya NHIF licha ya changamoto lukuki, wamesimama imara kuhakikisha uhakika wa matibabu kwa wote

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI imesema ipo mbioni kumaliza changamoto za bima binafsi zote za matibabu nchini na kwamba kwa kuanza itajumuishwa wakati wa kujadili sheria ya huduma ya Bima ya Afya kwa wote ambayo itajadiliwa na Bunge la Novemba, mwaka huu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Dkt. Dorothy Gwajima amesema hayo jijini hapa wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) huku akisema Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu kwa urahisi, kupitia sheria ya huduma za bima ya afya kwa wote na sheria hiyo itajadiliwa na wabunge ili ipate maoni na ridhaa kuelekea kuwa sheria.

"Serikali inatambua changamoto zilizopo kwenye mifuko ya bima binafsi,sheria itajadiliwa kuna mifuko ya Bima ya Afya ikiwemo Mifuko wa NHIF, Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), bima zote binafsi zitatazamwa kwenye sheria, wote watajumuishwa na kutazamwa ili kuwe na tija kwa watoa huduma wote," amesema.

Aidha, ametaka kuimarishwa kwa udhibiti kwenye eneo la udanganyifu na kuchukua hatua kwa watakaobainika na kusema kuwa tayari wizara yake imeanza kulifuatilia kwa uzito mkubwa suala hilo.

"Tumegundua wafamasia wengi wadanganyifu, wajiandae kujirudisha na wale wanataaluma wajiandae kujibu kwenye bodi na wakirudisha fedha tutakutathimini kama unafaaa kuwepo kwenye taaaluma au laa,"amesema.

Pamoja na hayo Waziri Gwajima ameeleza kuwa ili wananchi wapate huduma bora za bima ya afya lazima wanataaluma kuheshimu kazi na kuacha vitendo vya ubadhirifu na kwamba hakuna kituo kitakachofungwa ila watakaofanya ubadhirifu watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na hayo ametaka Mfuko wa NHIF nchini kuweka utaratibu mzuri wa kujisajili hasa maeneo ya vijijini ili wanachama waweze kujisajili na kuondokana na usumbufu uliopo kwa sasa.

Kutokana na hayo,aliyewahi kuwa Waziri wa Afya wakati mfuko huo unaanzishwa mwaka 2001,Anna Abdallah amesema utashi wa kisasa ulichangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa mfuko wa NHIF.

Amesema, licha ya ugumu uliokuwepo wa ushawishi kwa jamii kuhusu mfuko huo bado walisimama kwenye nguzo moja ambayo ndiyo iliwapa matumaini ya kutokata tamaa na kusababisha mafanikio yaliyopo sasa.

Ameeleza kuwa, mafanikio ya sasa yametokana na kuzikabili changamoto za mfuko huo na kuwa fursa.

"Watanzania wengi wanapenda kutumia Bima ya Afya hata sasa ukifika hospitali unaulizwa kama una kadi ya bima ni jambo la kujivunia sana,wakati tunaanza jambo hili wengi walidharau,ikifika wakati hata wale wenye bima walienda hospitali kutibiwa walinyanyapaliwa,sasa wanaheshimika,"amesema.

Amesema, japo safari mwanzoni ilikuwa ngumu lakini, mfuko unaendelea kufanya vizuri na kuwa njia za kisasa.

Mwenyekiti wa Bodi Mstaafu, Anna Makinda amesema, walipokuwa walianza walijibunia wataalam wa bima, lakini baadae waliambiwa mfumo hauzungumzi na sasa kuna Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

"Tunapokwenda ni kwema kwani leo mtu kama hana kadi ya bima anajilaumu," amesema.

Mmoja wa wajumbe wa bodi,Magreth Sitta amesema awali walimu walipinga ila ilisaidia zaidi kuboresha mfumo.

Ametumia nafasi hiyo kuitaka Serikali itoe elimu, watu waelewe zaidi watakavyonufaika na mfuko huo kwani wengine hadi sasa hawaelewi na kujikuta wanaenda kukata bima wakati wakiwa na wagonjwa nyumbani ,wakati kadi inapatikana baada ya mwezi moja.

Pia kwa maboresho zaidi ameshauri Serikali kupitia Wizara ya Afya iangalie namna ya kuhudumia wazee hasa wa vijijini kama dawa hakuna alipo ni mbali na mjini wanakosa matibabu na wengi wana changamoto ya umri.

Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya NHIF, Profesa Lucian Msambichaka amesema changamoto kubwa ilikuwa ni uelewa hasa kwenye suala la hisa huku akimtupia lawama Dkt. Gwajima kuwa alikuwa kikwazo wakati mfuko huo ulipoanza wakati huo akiwa Mganga Mkuu wa Singida.

"Mheshimiwa Waziri sikuteti,hata wewe ulitupa wakati mgumu wakati tunaaza,nashukuru baadaye ulituelewa na kukubali kutupa ushirikiano, wakati akiwa Mganga Mkuu Singida ulisaidia sana kutangaza fuko na Mkoa wa Singida ulifanya vizuri na kuwa mfano," amesema.

Amesema ,wananchi wengi hawakuwa na uelewa wa dhana nzima ya bima huku wengi wao wakiamini kuwa na Bima ya Afya mkononi ni sawa na kujitabiria magonjwa.

"Walipoambiwa walipie asilimia kadhaa waliona kama ni dhuluma, lakini kama bodi hilo halikutushangaza,tuliona kama jambo la kawaida,ealimu ndio walikuwa wagumu na tulichukulia kama changamoto," amesisitiza.

Prof.Msambichaka amesema, mfuko ulikuwa mchanga lakini Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa alisimama na mfuko ukaanza kutekekeza majukumu yake bila kuyumba.

"Wengi walikuwa hawaamini kama tutakwenda wenyewe bila utaalam kutoka nje, lakini marehemu Mkapa alisimama na kuwezesha zaidi msaada wa fedha na kusaidia kuondosha changamoto ikiwemo hospitali kupokea wagonjwa wenye bima na kuwapa kipaumbele,"amesema.

Hata hivyo amependekeza bodi na menejimenti ya NHIF wakamilishe mkakati endelevu kuelimisha wananchi juu ya Bima ya Afya ili wananchi wengi zaidi wajiunge na mfuko huo na kuwekeza zaidi kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Silvester Nyongo amesema wao kama wadau wa afya nchini wataendelea kuwa tayari kutoa ushirikiano na kuhakikisha wanafanikisha yale yote waliyopangwa.

"Kuna changamoto nyingi bado ziko kwenye Mfuko wa NHIF, lakini changamoto zake zinapelekwa Mfuko wa Afya ya Jamii CHF, jambo hili linatakiwa kuangaliwa,mzigo wa mfuko mwingine haupaswi kuhamishiwa kwenye mfuko mwingine,"amesisitiza.

Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa NHIF, Emmanuel Humba amesema mfuko umepitia changamoto nyingi wakati unaanzishwa, lakini sasa wanajivunia mafanikio ya mfuko na huduma nzuri zinatolewa na mfuko.

Kutokana na hayo ametaka kuendelea kutolewa kwa elimu zaidi ya bima ya afya na kuwezesha watanzania wengi zaidi wafaidike.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga amesema, kuna vituo vya afya 14,000 nchini ambavyo mfumo wa TEHAMA unafanya kazi hivyo kuwataka wateja wake kuwasilisha madai na malalamiko yao kwa kutumia njia ya TEHAMA.

Mkurugenzi huyo amesema, kwa sasa wanahudumia wanachama milioni 4.5 na wataendelea kuwekeza kwenye TEHAMA ili waweze kuhudumia wananchi wengi zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news