Mtaa wa Chinyika wapewa elimu ya chanjo ya UVIKO-19

Na Dennis Gondwe, DODOMA

CHANJO ya ugonjwa wa Uviko-19 imefanyiwa utafiti na nchi kujiridhisha kuwa ni salama ndiyo maana imeruhusiwa kutumika nchini ili kuokoa maisha ya watanzania.
Muuzugi Mfawidhi, Kituo cha Afya Mkonze,Lustika Mtaturu
Kauli hiyo ilitolewa na mtaalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Joseph Mdachi alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Mtaa wa Chinyika, Kata ya Mkonze jijini Dodoma katika siku ya pili ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo ya Uviko-19.

Chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19 imefanyiwa utafiti na Tanzania imejiridhisha kupitia wataalam wake kuwa ni salama ndiyo ikaruhusu iweze kutumika nchini. “Ndugu zangu, chanjo hii siyo ipo kwenye majaribio, imeshafanyiwa utafiti kabisa na kujiridhisha kuwa ni salama. Niwafahamishe tu kuwa dawa yoyote inapotumika, ikitokea ikasababisha shida au madhara, taarifa inatakiwa kutolewa kwa mamlaka kwa kujaza fomu maalum ili tatizo hilo liweze kufanyiwa kazi kitaalam. Lakini kwa chanjo hii hakuna tatizo lililobainika mpaka sasa kwa Jiji la Dodoma,” alisema Dkt. Mdachi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Chinyika, Kombo Ally Kombo alisema kuwa mtaa wake una bahati sana. “Serikali iliweka kutuo cha kupokea na kutibu wagonjwa wa Uviko-19 hapa. Na leo bahati nzuri tumeletewa chanjo hapa Kituo cha Afya Mkonze. Hii ni fursa kwetu kwa sababu hakuna foleni wakati wa kuchanja. Tutumie fursa hii kabla wengine wa mbali hawajaja kunufaika na fursa hii” alisema Kombo kwa kujiamini.

Nae Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkonze, Lustika Mtaturu alisema kuwa huduma za chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19 ni salama na inatolewa katika kituo hicho. Alisema kuwa kituo chake kimejipanga vizuri na wataalam wapo wa kutosha. Alisema kuwa timu ya wataalam itapita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuelimisha na kuhamasisha ili wananchi wahiari kuchanja.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Chinyika, Olympia Matoly alisema kuwa chanjo hiyo ni muhimu. “Napenda nitoe ufafanuzi, wataalam watakapo kuja nyumba kwa nyumba, watakuja kutoa elimu na kuhamasisha, ila kuchanja ni hiari. Wataalam watakapokuja tuwape ushirikiano mzuri,” alisema Matoly kwa msisitizo.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea na utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Uviko-19 kwa kutembelea taasisi mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha na kutoa huduma ya chanjo kwa watakaohamasika ikiwa katika siku yake ya pili.

Post a Comment

0 Comments