Serikali kuendeleza Mkakati wa Pamba hadi Nguo (C2C)

NA MWANDISHI MAALUM

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Pamba hadi Nguo (C2C) kupunguza uuzaji wa pamba ghafi nje ya nchi kutoka asilimia 70 kwenda 50 ili kuviwezesha viwanda vya uzalishaji nguo nchini kupata pamba ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji nguo kulingana na mahitaji ya soko.
Waziri Prof. Mkumbo ameyasema hayo alipotembelea Kiwanda cha Kuzalisha nguo cha NIDA kilichopo Tabata, jijini Dar es Salam Oktoba 16, 2021.

Katika kufungamanisha bidhaa za kilimo na viwanda vya uzalishaji, Prof. Mkumbo aliwaasa Wamiliki wa Viwanda vya kuzalisha nguo nchini kununua pamba ghafi ya wakulima inayolimwa katika mikoa 17 nchini kwa bei nzuri ili kuwavutia wasiuze pamba hiyo nje ya nchi bali wawauzie wao ili kukidhi mahitaji ya pamba ghafi katika Viwanda vyao.

Aidha, Waziri Prof. Mkumbo amesema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara ikiwemo urekebishaji wa sheria mbalimbali hasa inayohusu ajira kwa wageni viwandani kuwa Mgeni 1 kwa watanzania 10 na kutoka miaka 5 hadi 8 ili kurahisisha undeshaji wa mitambo inayotumia teknolojia ya kisasa na kuhuisha teknolojia ya uendeshaji mitambo hiyo kwenda kwa watanzania.

Prof. Mkumbo pia amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha Viwanda vinavyozalisha nguo vipate pamba ya kutosha kukidhi mahitaji yake ya pamba ghafi kwa ajili ya uzalishaji nguo nchini.

Naye, Meneja wa Uhusiano na ushauri wa Kisheia wa Kiwanda cha NIDA, Bw. Rajabu Honello amesema Serikali iendelee kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufaanyaji Biashara nchini kwa kulinda bidhaa za Viwand zinazozalishwa nchini kwa kuwa Viwanda hivyo vinatoa ajira nyingi na kuchangia katika pato la taifa wakati ikilinda wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Mingoni mwa Viwanda alivyotembelea Waziri Mkumbo ni pamoja na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za umeme cha Africab kilichopo kurasini na kiwanda cha NIDA ambacho kinazalisha bidhaa mbalimbali za nguo. Viwanda hivyo vinauza bidhaa zake Afrika Mashariki na Kati na barani Afrika kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments