Ujenzi barabara ya Kimara-Kibaha wafikia hatua za mwisho

NA MWANDISHI MAALUM

MRADI wa upanuzi wa Barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara-Kibaha kwa njia nane (kilomita 19.2), unaendelea vizuri na kwa sasa umefika asilimia 94.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoonwa na DIRAMAKINI Blog,mradi huo unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia mia moja na gharama yake ni takriban Shilingi Bilioni 161 huku ukitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba, mwaka huu.

Aidha, Serikali imeshamlipa Mkandarasi malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 149. 8 ambazo ni sawa na asilimia 93 kulingana na kazi aliyoifanya.

Hadi sasa kazi zilizobakia ni kuweka taa za kuongozea magari, taa za kuangaza barabarani, kuweka kingo (kerbstobne) na kutenga njia zinazoelekea mjini na zinazotoka mjini na kumalizia lami kipande cha kilometa 4 kutoka eneo la Gogoni- Kibamba hadi Kibaha.

Mradi huu unatekelezwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), ambapo lengo lake kubwa ni kupunguza msongamano kwa wasafiri na wasafirishaji wanaongia katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Aidha,kukamilika kwa mradi huu kutaunganisha nchi yetu na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Malawi.

Mradi huo ulianza mwaka 2018 na unajengwa na Kampuni ya kikandarasi ya Estim kutoka Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news