WANANCHI MIHAMBWE WAJITOKEZA KUIUNGA MKONO SERIKALI

Na Mwandishi Wetu,Mihambwe

Wananchi wa Tarafa ya Mihambwe wamejitokeza kwa wingi kuiunga mkono Serikali kwenye hatua ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yanayotokana na fedha za mpango wa maendeleo na ustawi wa jamii dhidi ya mapambano ya uviko 19.
"Namshukuru sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kutuletea mradi huu na sisi Wanakijiji tumejitolea nguvu kazi kufanikisha mradi huu,"amesema Mwajuma Ali mkazi Kijiji cha Mwenge A.

"Tunaishukuru Serikali kutuletea fedha ujenzi madarasa haya, tunahaidi kuyasimamia mpaka kufikia lengo." Alisema Hanafi Athumani Navanga mkazi kata ya Kitama.

Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya kufuatilia utekelezaji miradi ya ujenzi wa Madarasa iliyofanywa na Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ambapo aliwashukuru sana Wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kutoa nguvu kazi zao la uchimbaji misingi ya ujenzi wa Madarasa hayo.

"Tunawashukuru sana Wananchi mnavyojitolea nguvu kazi sana zenu. Hii ni ishara nzuri ya umoja, mshikamano na upendo mnaoonyesha kwa Serikali. Nguvu kazi yenu mnayojitolea itasaidia kuweka Madawati na hata ikiwezekana kuanzisha mradi mwingine ama kumalizia iliyokwisha anza. Tunawahaidi Serikali kuwa wawazi na kuwashirikisha Wananchi kwenye kila hatua. Lengo mradi ukamilike kwa Wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha,"amesisitiza Gavana Shilatu.

Gavana Shilatu alipita kwenye maeneo mbalimbali kufuatilia utekelezaji ujenzi wa Madarasa hayo kwa kushiriki uchimbaji misingi ambapo maeneo mbalimbali wamefanikisha hatua ya uchimbaji misingi na ujenzi unaendelea kwa kasi.

Post a Comment

0 Comments