Man City yapiga tatu, yaondoka na alama tatu kwa Everton

NA GODFREY NNKO

PENGINE mashabiki wa Everton wanawatazama Raheem Sterling, Rodri na Bernardo Silva wa Manchester City kama adui, ni baada ya kuwabamiza na kitu kizito.
Nyota wa Manchester City, Rodri akifurahi baada ya kuwapa zawadi ya ushindi waajiri wake dhidi ya Everton. (Picha na Getty Images).

Ni dakika ya 44 ndiyo Raheem aliitumia kuwaonyesha Everton kuwa, wametumwa ushindi tu, baada ya kutumbukiza nyavuni bao.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko, ambapo moto wa Manchester City uliendelea kuwaka kipindi cha pili baada ya Rodri ndani ya dakika ya 55 kuwaacha midomo wazi mashabiki wa Everton wasijue kilichotokea kwa kupachika bao la pili.

Aidha, bao hilo lilidumu hadi dakika ya 86 ambapo Everton huku wakitafuta namna ya kujinasua walijikuta wakiingia tena majaribuni baada ya Bernardo kupachika bao la tatu ambalo lilidumu hadi dakika ya mwisho.

Kupitia mtanange huo uliopigwa katika dimba la Etihad ukiwa ni mwendelezo wa mitanange ya Ligi Kuu ya England (EPL), Novemba 21, 2021 vijana wa Pep Guardiola waliondoka na alama zote tatu zikisindikizwa na mabao matatu.

Huku Everton wakiondoka vichwa chini, wao Man City kwa matokeo hayo wanafikisha alama 26 wakiwa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, wakizidiwa tatu na Chelsea baada ya wote kucheza mechi 12 huku vijana wa Rafael Benítez Maudes wakiwa nafasi ya 11 na alama zao 15 wakiwa wamecheza mechi 12.

Post a Comment

0 Comments