Miaka 60 ya Uhuru:REA yarekodi mafanikio ya kihistoria katika kuwafikishia wananchi umeme vijijini

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesema imevuka malengo iliyojiwekea ya asilimia 50 katika kuwafikishia wananchi huduma ya umeme viijini ambapo hadi kufikia Juni 2021 asilimia 69.6 ya vijiji vilikuwa vimefikiwa na huduma hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Novemba 30,2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Hassan Saidy ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa REA ameyasema hayo leo Novemba 30,2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa,   wakati Taifa linaelekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hali ya maisha ya wakazi wa vijijini imebadilika ambapo mwaka 2007 wakati eakala inaanzishwa ni asilimia mbili tu ya vijiji vilikuwa vimefikiwa na huduma ya umeme.

“Kuna mafanikio mengi tuliyoyapata kutokana na usanifu, utekelezaji na usimamizi wa miradi inayotekelezwa na wakala tangu kuanziswa kwake ambapo miradi hiyo imewezesha ujenzi wa jumla ya kilomita 38,296.56 za umeme msongo wa kati na kilomita 35,253.43 za umeme msongo mdogo.

"Lakini pia kuna jumla ya wateja 716,847 waliounganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 2,661.93 kwa kipindi cha miaka 14 tangu kuanzishwa kwake,"amesema Mhandisi Saidy.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kutengeneza masoko kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa miradi ya umeme.

Pia kuwezesha uboreshwaji wa kilimo cha umwagiliaji katika mashamba likiwemo shamba la Mtakuja Kilimanjaro na Zuzu Dodoma.

Mhandisi Saidy ametaja mafanikio mengine kuwa ni kufunga mifumo ya umeme katika nyumba za wafanyakazi takribani 831 kwenye sekta ya afya na elimu katika mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Kagera, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Tabora.

Wakati huo huo, Mhandisi Saidy amesema, hagua hiyo imewezesha kuboresha mazingira ya makazi vijijini ambayo imepelekea kupunguza uhamiaji wa vijana kutoka vijijini kwenda mjini kwa kuwa umeme umewamewezesha kufanya shughuli za kiuchumi kwenye makazi yao.

“Vijana wengi sasa wanatulia vijijini kwani wameweza kuanzisha viwanda vidogo na vya kati katika juhudi za kujikwamua kiuchumi. Vitu kama vile mashine za kusaga, kuchomelea, viwanda vya useremala pamoja na saluni za kike na kiume vinapatikana hadi vijijini siku hizi.

"Lakini pia upatikanaji wa taarifa na burudani kwa wepesi kama vile televisheni na redio vimeongeza utulivu kwa vijana wengi hapa nchini,"ameongeza Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy alieleza sababu za kuanzishwa kwa mpango huo wa REA kuwa ni kuhamasisha, kuratibu na kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa miradi ya nishati bora vijijini ili kuhakikisha kuwa nishati bora vijijini inachangia ukuaji uchumi na kuboresha huduma za jamii.

Amesema, hadi  sasa wameweza kutekeleza miradi 21, kati ya miradi hiyo 13 ni ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji, saba kwa njia ya jua huku mmoja wa kutumia tungamo taka (bayogesi).

Amesema, REA inatarajia hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha ujao takribani vijiji vyote 12,345 vitakuwa vimeunganisha umeme kwa awamu ya tatu.

Mhandisi Saidy amesema,  wameweza kuunganisha umeme kwa taasisi za elimu zipatazo 7,735, vituo vya afya 402, maeneo mbalimbali ya biashara 1,967 pamoja na nyumba za ibada 5,117.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa umeme, Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila amesema kwamba katika kuhakikisha mtu mmoja mmoja anafaidika na uwepo wa umeme, Serikli inahamasisha wananchi wengi waone umuhimu wa kuunganishiwa umeme kwenye makazi yao ili kufaidi fursa zinazoletwa na nishati hiyo.

“Tunaondoka kwenye hatua ya kuhakikisha umeme unafika kijijini, na hivi sasa tunawahamasisha wakazi wa eneo husika kuhamasika kuunganishiwa umeme huo kwenye makazi yao. Mwamko ni mkubwa na tunapokea maombi mengi na hivi sasa tunahamasisha ushiriki wa sekta binafsi, taasisi za fedha katika uwekezaji wa miradi ya nishati vijijini na tunaendelea kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu kutoka vyanzo vya asili vinavyopatikana maeneo ya vijijini na kwenye visiwa,"amesema Mhandisi Rwebangila.

Pia Mhandisi huyo amesema kwa sasa wanaendelea na mradi wa kuunganisha umeme wa jua (sola) katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo mpango ni kuhakikisha kunakuwa na miradi mingi ya sola ili kuhakikisha nishati ya kutosha inapatikana wakati wote.

Wakala wa Nishati Vijiji ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Nishati Vijijini Na. 8 ya mwaka 2005 na kuanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake mwezi Oktoba, 2007 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa iliyokua Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2003.

Post a Comment

0 Comments