Milioni 950/- zatengwa kujenga vituo viwili vya afya Songea

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI imetenga shilingi milioni 950 wa ajili ya kujenga vituo viwili vya afya katika Kata ya Msamala na Lilambo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ikiwa ni mkakati wake wa kusogeza huduma za matibabu kwa wananchi wa kata hizo karibu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akikagua ubora wa mawe yanayotumika kwenye mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Msamala katika Manispaa ya Songea mkoani humo kwa gharama ya shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali kwa lengo la kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa kata hiyo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Dkt.Frederick Sagamiko ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa Kituo cha Afya Msamala kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.

Amesema, kati ya fedha hizo shilingi milioni 500 zitatumika kujenga Kituo cha Afya Msamala na shilingi milioni 450 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya Lilambo kata ya Lilambo.

Dkt.Sagamiko amesema,mradi wa ujenzi wa Kituo cha Msamala umeibuliwa na wananchi wenyewe kwa madhumuni ya kupunguza kero ya kutembea umbali mrefu hadi kituo cha afya Mjimwema na Hospitali ya rufaa Songea kufuata matibabu.

Dkt.Sagamiko amesema,ujenzi wa mradi huo utahusisha jengo la maabara,upasuaji,jengo la wagonjwa wa nje,wodi ya wanawake,choo cha nje,kichomeo taka,shimo la kondo na shimo la maji taka.

Pia amesema katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali imetoa shilingi milioni 500 ambapo wananchi wa kata hiyo wamechangia kiasi cha shilingi milioni mbili na unatekelezwa kwa mfumo wa force account na umewezesha wananchi hasa wanaoishi kata hiyo kushiriki katika shughuli za ujenzi na kujipatia kipato.

Dkt.Sagamiko ametaja manufaa ya mradi huo mara utakapokamilika ni upatikanaji wa huduma bora ya mama na mtoto na hivyo kupunguza vifo vya akina mama na mtoto kutoka 202 hadi 190 kwa vifo 100,000 kwa mwaka.

Aidha, faida nyingine ni upatikanaji wa huduma ya dharura ya upasuaji kwa akina mama wajawazito,kupungua kwa magonjwa ya kuambukiza na yasioambukiza pamoja na wananchi watapa elimu ya lishe,hivyo kupunguza tatizo la utapiamlo kwa watoto.

Huduma nyingine zitakazopatikana ni chanjo,huduma ya tohara huduma ya upimaji wa VVU/Ukimwi na kuzuia maambukizi pamoja na kupunguza mzigo wa wagonjwa uliokuwa unaielemea Hospitali ya mkoa na kituo cha afya Mjimwema.

Amesema, katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Manispaa hiyo imepanga kutumia shilingi milioni 450,000,000.00 ikiwa ni fedha za mapato ya ndani kujenga kituo cha Afya Lilambo na wananchi wamechangia shilingi milioni 3,295,000.00 ambapo shilingi milioni 160,000,000.00 zimetolewa kutekeleza kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amemtaka fundi anayesimamia mradi huo kuhakikisha unajengwa kwa viwango na unakamilika kwa wakati ili uweze kuleta tija kwa wananchi ambao walisubiri mradi huo.

Amesema,lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuwatatua kero wananchi zilizokuwepo ikiwemo huduma za matibabu,ambapo amewapongeza wananchi wa Kata ya Msamala kwa kuibua mradi huo na kushiriki katika shughuli za ujenzi.

Brigedia Jenerali Ibuge amesema,Serikali ya mkoa itakuwa bega kwa bega na wananchi hao na kufuatilia kwa karibu mradi huo ili ukamilike haraka.

Naye Diwani wa Kata ya Msamala, Michael Mbano amesema, Kata ya Msamala ni kubwa na yenye wakazi wengi,hata hivyo kwa muda mrefu haikuwa na huduma zozote za matibabu badala yake wananchi walilazimika kwenda kutibiwa hospitali ya mkoa na kituo cha afya Mjimwema.

Post a Comment

0 Comments