Sepp Blatter,Michel Platini watuhumiwa kupiga mabilioni ya FIFA, UEFA

NA GODFREY NNKO

Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA),Sepp Blatter mwenye umri wa miaka 85 na Rais wa zamani wa Muungano wa Mashirikisho ya Soka Barani Ulaya (UEFA), Michel Platini mwenye umri wa miaka 66 wametuhumiwa kutumia vibaya ofisi.
Sambamba na kusababisha upotevu wa fedha za Kitanzania shilingi bilioni 7.4 (sawa na Franka za Uswisi-dola milioni 2.94)

Hayo yamebainishwa Novemba 2, 2021 na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka (OAG) wa Uswisi.

Kupitia tuhuma hizo, inaelezwa kuwa aliyekuwa Rais wa FIFA, Blatter alirasimisha muamala wa fedha hizo ambazo zilielekezwa kwa Platini mwaka 2011, jambo ambalo halipo kwenye mpango.

Aidha, kwa mujibu wa mwendesha mashtaka,matumizi ya ofisi vibaya yaliharibu taswira ya shirikisho pamoja na kumtajirisha Platini kinyume na utaratibu wa kawaida.

Vigogo hao baada ya kutuhumiwa watatakiwa kufika katika Mahakama ya Shirikisho inayoshughulikia uhalifu iliyopo mjini Bellinzona, Uswisi.

"Malipo haya yaliharibu taswira ya FIFA na kumtajirisha Platini kinyume cha sheria," ilieleza taarifa ya mwendesha mashtaka.

Kesi hiyo ilifunguliwa Septemba 2015 na kupelekea Blatter kuondolewa madarakani kabla ya muda uliopangwa kuwa rais wa FIFA. Pia ilihitimisha kampeni ya rais wa wakati huo wa UEFA, Platini kumrithi mshauri wake wa zamani.

Haya yanajiri baada ya hatua mbalimbali kufuatwa ambapo kesi za Uswisi mara nyingi huchukua miaka kadhaa kufikia hitimisho.

Kesi hiyo inahusu ombi la maandishi la Platini kwa FIFA mnamo Januari 2011 kulipwa mshahara wa awali wa kufanya kazi kama mshauri wa rais katika muhula wa kwanza wa Blatter, kuanzia 1998-2002.

Blatter aliidhinisha FIFA kufanya malipo hayo ndani ya wiki chache. Alikuwa akijiandaa kufanya kampeni ya kuchaguliwa tena katika kinyang'anyiro dhidi ya Mohamed bin Hammam wa Qatar, ambapo ushawishi wa Platini kwa wapiga kura wa Ulaya ulikuwa jambo kubwa.

"Ushahidi uliokusanywa na (ofisi ya mwanasheria mkuu) umethibitisha kwamba malipo haya kwa Platini yalifanywa bila msingi wa kisheria,"taarifa ya mwendesha mashtaka iliongeza.

Blatter amefunguliwa mashtaka ya ulaghai, matumizi mabaya ya fedha, matumizi mabaya ya fedha za FIFA na kughushi hati.

Platini ameshtakiwa kwa makosa ya ulaghai, matumizi mabaya ya fedha, kughushi na kama mshiriki wa madai ya usimamizi mbovu wa Blatter.

Hata hivyo, endapo itabainika kuwa tuhuma hizo ni kweli, vigogo hao wawili wanaweza kuadhibiwa kwenda jela kwa miaka kadhaa au faini licha ya wote kwa pamoja kukanusha tuhuma hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news