Hereni za kielektroniki kwa mifugo kote nchini kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ikiwemo ngozi

NA EDWARD KONDELA

UONGOZI wa Mkoa wa Geita umesema uwekaji hereni za kielektronoki kwa mifugo kote nchini hususan katika mkoa huo utasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ikiwemo ngozi ambayo imekuwa ikiharibiwa kwa kuweka alama kwa njia ya moto kwenye ngozi ya mnyama.
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki mkoani Geita, Katibu Tawala wa mkoa huo, Dkt. David Misonge amesema ngozi ya mnyama imekuwa ikiharibiwa na kufanya zao la ngozi kushuka thamani na lisiweze kutumika katika matumizi mbalimbali kwa kuwa inakuwa imeharibiwa kwa kuwekewa alama nyingi.

Amesema, ni muhimu kwa wafugaji wa Mkoa wa Geita kuunga mkono zoezi hilo ili mifugo iwe na thamani zaidi na kuweza kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi na kuliongezea zaidi thamani zao la ngozi.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Dkt. David Misonge akizungumza na baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na mwakilishi wa Kampuni ya S & J iliyopewa zabuni ya kutengeneza hereni za kielektroniki kwa ajili ya mifugo na kuzisambaza kote nchini. Maafisa hao wameongozwa na Dkt. Audifas Sarimbo kutoka Idara ya Huduma za Mifugo, wakati walipofika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa ajili ya kutambulisha mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki.

Naye afisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Idara ya Huduma za Mifugo,Dkt. Audifas Sarimbo akizungumza kando ya mkutano huo baada ya kutoa maelezo ya mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki katika mkutano huo uliohudhuriwa na maafisa kutoka Idara ya Mifugo na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mkoa wa Geita na wilaya zake, amesema baadhi ya wafugaji katika Mkoa wa Geita wamekuwa hawatilii maanani sana thamani ya mifugo kutokana na uwepo wa madini ya dhahabu licha ya kuwa mkoa huo una mifugo mingi.

Dkt. Sarimbo ameongeza kuwa, uwekaji wa hereni za kielektroniki kwa mifugo pamoja na utoaji wa elimu ya kuthamini mifugo hiyo kutasababisha wafugaji wa Mkoa wa Geita kuthamini zaidi mifugo yao ikiwemo kuacha kuweka alama kwa mnyama kwa njia ambazo zinaharibu ngozi.

Akizungumza kwa niaba ya mzabuni anayetengeneza na kusambaza hereni za kielektroniki kwa ajili ya mifugo Kampuni ya S & J, Mkurugenzi wa Kampuni ya LERACO Bw. Shangilia Lema amesema, hereni za kieletroniki zina uwezo wa kudumu kwa muda mrefu na kwamba hazitoki kirahisi kwa mnyama baada ya kuwekewa kwenye sikio, huku baadhi ya wafugaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita waliofikiwa na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kupatiwa elimu juu ya hereni za kielektroniki wakipongeza zoezi hilo kwa kuwa litaongeza thamani ya mifugo yao pamoja na kuzuia wizi wa mifugo.

Zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa hereni za kielektroniki ambalo linafanyika kote nchini kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2011 linatekelezwa kwa mfugaji kulipia gharama ya Shilingi 1,750 kwa ng’ombe na punda na Shilingi 1,000 kwa mbuzi na kondoo.

Post a Comment

0 Comments