Rais Dkt.Mwinyi aridhia masahihisho ya muundo wa utumishi SUZA

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakubaliana na hatua zilizoanza kuchukuliwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika kuufanyia masahihisho muundo wa utumishi ili kuhakikisha wahadhiri na wafanyakazi wa chuo hicho wanalipwa kwa mujibu wa nafasi zao, muda na kiwango cha elimu. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwatunuku Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, watika wa hafla ya mahafali ya 17 ya chuo hicho yaliofanyika katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.(Picha na Ikulu).  

Dkt.Mwinyi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), amesema hayo katika Mahafali ya 17 ya chuo hicho, yaliofanyika katika Ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein, uliopo Tunguu Mkoa Kusini Unguja. 

Amesema, kwa kutambua juhudi zinazofanywa na wahadhiri na wafanyakazi wa chuo hicho, Serikali inakubaliana na hatua zilizoanza kuchukuliwa na Uongozi wa chuo hicho katika kuangalia upya na kuufanyia masahihisho muundo wa utumishi ili kuhakikisha kila mmoja anapata stahiki zake kwa mujibu wa nafasi, muda wa utumishi na kiwango cha elimu. 

Alieleza kuwa , Serikali inatambua kuwepo kwa taratibu za upandaji wa madaraja kwa taasisi za elimu nchini, hivyo akabainisha suala hilo kuzingatiwa kikamilifu. 

Aidha, alisema Serikali ina azma ya kushirikiana na uongozi wa chuo hicho pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika kuitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa wahadhiri na watumishi wengine wa chuo hicho, ili kuziba nafasi zilizo wazi kufuatia hatua ya Serikali ya kuwateua wahitimu wengi kushika nafasi mbalimbali za uongozi Serikalini. Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wakati wa hafla ya Mahafali ya 17 ya Chuo hicho yaliofanyika katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.(Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi aliutaka uongozi wa SUZA kuandaa utaratibu mzuri wa kupata wahadhiri miongoni mwa waihitimu wake bora, sambamba na kuwaendeleza wahitimu waliopo na watumishi wa kada nyingine, kwa kuandaa program maalum za mafunzo ili kupanua wigo na kuwawezesha wale wenye sifa na ambao bado hawajapata mafunzo; kupata nafasi hizo. 

Amesema , uongozi wa chuo hicho una wajibu wa kutafuta njia mbadala za kupata fedha  ikiwemo mikopo na kuanzisha miradi ya maendeleo iyakayokiletea faida chuo hicho, na akibainisha kuwa mfumo wa aina hiyo umekuwa ukitumiwa na vyuo mbalimbali duniani kama njia ya kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya aina mbalimbali ya chuo. 

“Nikupeni moyo kuwa Serikali ipo tayari kutoa dhamana , kwa taasisi za fedha kwa mikopo ambayo tutajiridhisha itakisaidia chuo kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo,”amesema. 

Alieleleza kuwa, chuo kikuu ni taasisi na kiungo cha ushirikiano kati yake na watu, hivyo akatoa wito wa kuwa na mashirikiano na vyuo vikuu vingine ili kujifunza mambo mapya, kubadilishana uzoefu, kushirkiana katika masuala mbalimbali ya kitaaluma pamoja na kufanya tafiti. 

Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi aliwapongeza wahitimu wote, hususan wa kike kwa kuwa na idadi kubwa ya wahitimu, ikilinganishwa na wanaume pamoja na kushika nafasi nyingi za juu katika masomo mbalimbali. 

Amewataka wahitimu wote kutotosheka na ngazi ya elimu waliyofikia na badala yake kuanza juhudi za kujiendeleza zaidi kimasomo pamoja na kuwataka kuitumia vyema taaluma waliyopata katika kujiletea mabadiliko na kujiajiri au kuajiriwa kwa kuzingatia sifa na uwezo walionao. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Mahafali ya 17 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliofanyika katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.(Picha na Ikulu). 

Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohammed Said amesema, wizara hiyo ina azma ya kujenga ukaribu na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili kuwawezesha vijana wanaohitimu kuweza kuingia katika soko la Ajira katika maeneo tofauti Duniani. 

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Khamis akiwa pia ni Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, alisema katika mwaka wa masomo 2020/2021 Baraza limeweza kusimamia uendeshaji, wajibu na haki za wahadhiri na wafanyakazi wa chuo hicho, ikiwemo suala la upatikanaji wa stahiki zao pamoja na upandishaji wa madaraja. 

Alieleza kuwa, baraza hilo lilipata fursa ya kujadili na kuchambua changamoto mbalimbali zinazowahusu wahadhiri na wafanyakazi wa chuo ili kuhakikisha ufanisi wa kitaaluma unapatikana, ikiwemo suala la kupishana sana kwa mishahara. 

Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Mohamed Makame Haji alisema mafanikio ya chuo hicho ya kuendelea kutoa idadi kubwa ya wahitimu kuwa sio jambo la kubahatisha, bali linatokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu nchini. 

Amesema, mafanikio hayo yanatokana na umoja na mashirikiano ya wadau wote wa elimu, ikihusisha Uongozi wa SUZA pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. 
Baadhi ya viongozi wa Serikali na wageni waalikwa wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika hafla ya Mahafali ya 17 ya Chuo Kikuu cha SUZA yaliofanyika katika ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.(Picha na Ikulu).

Alieleza kuwa, katika mwaka huo wa masomo (2020/2021) chuo hicho kilikabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ya kutokuwa na Dakhalia za kutosha katika baadhi ya Skuli zake pamoja na kutokuwa na miundombinu bora katika baadhi ya Dakhalia. 

Vile vile alisema kumekuwepo mrundikano mkubwa wa wahadhiri katika baadhi ya Skuli na taasisi za Chuo hicho, ikiwemo Chuo cha uongozi wa Fedha Chwaka. 

Katika mahafali hayo, jumla ya Wahitimu 1894 wa fani na ngazi mbali walitunukiwa Vyeti, Stashahada, Shahada, Shahada za Uzamili pamoja na Shahada za Uzamivu kutoka taasisi na Skuli mbalimbali za chuo hicho, ikiwemo Skuli ya Kilimo, Skuli ya Kompyuta,Mawasiliano na Taaluma ya Habari,Skuli ya Biashara na Taasisi ya Utalii. 

Nyingine ni Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Skuli ya Elimu, Skuli ya Sayansi Asili na Sayansi Jamii na Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni. 

Aidha, katika hafla hiyo Rais Dkt.Mwinyi alitunuku zawadi kwa wanafunzi bora waliofanya vizuri zaidi katika masomo mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments