Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya aguswa na fursa za uwekezaji Tanzania

NA KASSIM NYAKI, UAE 

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) Aleksander Čeferin ametembelea banda la Tanzania katika maonesho ya Kimataifa ya Dubai EXPO 2020 yanayoendelea katika Nchi za Falme za Kiarabu ambapo ameonesha kufurahishwa na fursa za uwekezaji zilizoko nchini Tanzania. 

Čeferin ametoa kauli hiyo baada ya kupata maelezo kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania katika sekta za kilimo, utafiti, Madawa na Vifaa tiba, Maliasili na Utalii, teknolojia, uzalishaji wa Sukari na usindikaji wa mazao katika sekta mbalimbali ambazo ni kichocheo cha uchumi wa Tanzania.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya Aleksander Čeferin ( aliyevaa tisheti nyekundu) akimsikiliza Afisa Uhamasishaji Uwekezaji Mwandamizi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Latiffa Kigoda (kulia) kuhusu fursa za uwekezaji zilizoko Tanzania. wa pili kulia ni mkurugenzi wa Banda la Tanzania EXPO 2020 Dubai Bi Getrude Ng’weshemi.

“Nimewahi kuja Tanzania na Kutembelea maeneo ya vivutio kama Hifadhi za Ngorongoro, Serengeti na Mlima Kilimanjaro, leo nimejua zaidi kuwa Tanzania pia ina mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali, hii ni baraka na neema ambayo wageni wanaokuja kwenye maonyesho haya wanapaswa kutembelea banda hili kupata maelezo kuhusu vivutio vya utalii, uwekezaji na kujua uwepo wa madini mbalimbali ambayo mengine yanapatikana Tanzania pekee” amefafanua Čeferin 

Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika maonesho hayo Bi. Getrude Ng’weshemi amemueleza Rais wa UEFA kuwa katika jitihada za kuboresha mazingira ya uwekezaji, Tanzania inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutokea bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuunganisha na nchi jirani na uboreshaji wa miundombinu katika Sekta ya Utalii. 
Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika maonesho ya Dubai EXPO 2020 Getrude Ng’weshemi (wa pili kutoka kulia) akimueleza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya (UEFA) Aleksander Čeferin ( aliyevaa tisheti nyekundu) kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania. 
Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika maonesho ya Dubai EXPO 2020 Getrude Ng’weshemi (aliyenyoosha mkono) akimueleza Rais wa Shirikisho la Mpira wa miguu Barani Ulaya (UEFA) Aleksander Čeferin ( aliyevaa tisheti nyekundu) akionyeshwa sehemu ya mazao ya kimkakati yaliyopo Tanzania. Kulia ni Afisa Uhusiano kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Kassim Nyaki.

“Tanzania inazungukwa na nchi zaidi ya 8 zikiwemo Uganda, Rwanda, Sudani ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Zambia na Malawi, na sehemu kubwa nchi hizi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam na ndio maana serikali inatumia jitihada kubwa kuboresha Bandari hiyo ya pamoja na miundombinu ya Reli ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wa bidhaa na mizigo” aliongeza Bi. Getrude 

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bi. Latiffa Kigoda amemueleza Rais wa UEFA na ujumbe wake kuwa Nchi ya Tanzania inakaribisha wawekezaji katika sekta za kilimo na uongezaji thamani mazao, uzalishaji wa mafuta ya kula, uzalishaji wa sukari, nguo, uzalishaji wa madawa na vifaa tiba, mifugo na uongezaji thamani katika uzalishaji wa maziwa, usindikaji wa nyama na utengenezaji wa bidhaa za ngozi, uvuvi na usindikajj wa samaki, uzalishaji wa mbolea, na uanzishaji wa maeneo ya ukanda maalum ya uwekezaji ‘’industrial parks”. 
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya Aleksander Čeferin ( aliyevaa tisheti nyekundu) akiangalia madini aina ya Tanzanite yanayozalishwa Tanzania pekee wakati wa ziara yake ya kutembelea banda la Tanzania katika maonesho ya Dubai EXPO 2020 Dubai yanayoendelea katika Jiji la Dubai Nchi za Falme za Kiarabu.

Bi Latiffa ameongeza kuwa Ili kumrahisishia mazingira ya uwekezaji Tanzania, Serikali imeanzisha Mfumo wa huduma za pamoja (One Stop Facilitation Centre), ambapo Maafisa Waandamizi wa Taasisi mbalimbali za Serikali wanasaidia mwekezaji kupata vibali, leseni na idhini katika sehemu moja (one stop Centre). 

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni TIC, Wizara ya Ardhi, TANESCO, BRELA, TRA, NEMC, OSHA, TMDA, NIDA, Uhamiaji, Wizara ya Kazi na TBS. 

Miongoni mwa taasisi za Tanzania zinazoshiriki maonyesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Abu Dhabi katika Nchi za falme za Kiarabu. 

Maonesho hayo ya kimataifa yaliyoanza tarehe 01 oktoba, 2021 yanaendelea hadi mwishoni mwa mwezi Machi, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news