Wahabeshi 51 wakamatwa jijini Dodoma wakisafirishwa katika gari la mizigo

NA DOREEN ALOYCE

JESHI la Polisi jijini Dodoma limewatia mbaroni wahamiaji haramu 51 raia wa Ethiopia na watu wawili raia wa Tanzania waliokuwa wakisafirishwa katika gari la mizigo wakitokea Kanda ya kaskazini kuelekea mikoa ya Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 28 jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Onesmo Lyanga amesema kuwa, watuhumiwa hao wamekamatwa tarafa ya Bereko Wilaya ya Kondoa wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T.593 AUE aina ya fuso likiendeshwa na Ignas Mgosi (23) mkazi wa Mafinga akisaidiwa na Jafari Idd (39) mkazi wa Arusha.

“Askari walipekua gari hilo na kuwakamata wahamiaji hao raia wa Ethiopia wakitokea Moshi Kilimanjaro kwenda Iringa, mbinu iliyotumika ni kuwaficha kwa turubai, kiini cha tukio ni kukosa uzalendo wa nchi na tamaa mbaya ya kujiptia kipato isivyo halali,” amesema Kamanda Lyanga.
Aidha, ametoa wito kwa vijana wa kitanzania na madereva na wamiliki wa magari kuwa waache tamaa ya kufanya vitendo vya uhalifu kwa kuwa uhalifu haulipi.

“Kwa mujibu wa sheria ya nchi kifungu 46 (1) (a) – (g) cha sheria ya uhamiaji sura ya 54 siyo tu watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kupata hukumu ya kifungo bali ni pamoja na gari lililohusika kufirisiwa na wamiliki kupata umasikini,”amesema Lyanga.
Kwa upande wake Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Kaimu Afisa Uhamiaji, Adam Mkuyu amesema wamejipanga kila kona kuhakikisha hakuna mhamiaji anaingia kinyemela.

“Sisi uhamiaji tumejipanga kila sehemu kuhakikisha vitendo hivi vya uhamiaji haramu tunavipiga vita vikali, lakini pia nitoe wito kwa wenzetu ambao wanahitaji kuhamia nchini kwetu wafuate sheria na kanuni za uhamiaji,"amesema Mkuyu.

Post a Comment

0 Comments