Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete aridhishwa na ufanisi wa NHC, asisitiza dhamira ya Rais Samia

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kulijengea uwezo zaidi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili liweze kutekeleza miradi yake mikubwa, kimkakati na mingineyo kwa manufaa ya Taifa na wananchi wake.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ameyasema hayo Januari 24, 2022 baada ya kufanya ziara makao makuu ya NHC na kutembelea moja wapo ya mradi wa kimkakati wa Morocco Square uliopo jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Ridhiwani amesema kuwa, lengo kuu la ziara yake ni kulitambua na kulisoma vizuri Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na jinsi gani wanafanya kazi.

Pia kutambua changamato ambazo wanakabilia nazo, kwani maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni mawaziri kuhakikisha mambo yote ambayo yanafanyika katika Serikali hayakwami.

"Na (Mheshimiwa Rais) anatutaka, tuwe 'solution oriented ministers', Siyo mawaziri ambao mnakwenda kazi yenu mnapiga piga tu maneno, kwa hiyo katika siku ya leo ambalo tumelifanya, kwanza ni kukutana na menejimenti ya shirika, ikiongozwa na bodi yao. Tumekutana kwa pamoja na kuweza kufanya mazungumzo ya kina sana juu ya shirika linaendeshaje shughuli zake kwanza. Pili kama kuna mikwamo yoyote katika shirika hili, kwani shirika linafanya kazi nyingi sana, linafanya miradi mingi.

"Walipata nafasi ya kunieleza juu ya maeneo ambayo wanayafanyia kazi na mifumo ambayo wanaifanyia kazi,kwa hiyo nimewaelewa sana, lakini pia pamoja na hayo nilipata nafasi ya kuelekezwa kuhusu miradi ambayo wanaifanya, kwa hiyo nikawaambia kwa siku ya leo, moja ya miradi mikubwa ambayo ninataka kwenda kuuona ni wa Morocco Square.

"Kwa sababu mradi huu una sifa nyingi, ukiachia miradi mingi waliyonayo, mradi huu ni moja ya miradi ambayo ina sura ya kipekee, kama mnavyojua hii Junction ya Morocco ni moja wapo ya Junction kubwa sana katika maeneo ya makutano katika Dar es Salaam hii,"amesema Mheshimiwa Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete.
Mradi wa Morocco Square uliopo katika makutano ya Barabara ya Mwai Kibaki na Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam ambao unatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 137.5 ambapo ukikamilika unatarajiwa kutoa huduma za nyumba za makazi kwa ajili ya kuuza na kupangisha.

Pia unatarajiwa kutoa huduma za maduka makubwa, ofisi, kumbi za sinema, benki na hoteli ambapo hadi sasa umefikia asilimia 93 kabla ya kukamilika.

"Binafsi yangu nimshukuru sana Mkurugenzi Mkuu na Bodi yake kwa namna ambavyo imenipa ushirikiano mkubwa katika kuuona mradi huu. Binafsi yangu Mkurugenzi niseme nimeridhika na mazingira niliyoyaona, changamoto tulizoziona hapa ni jukumu letu Serikali kama alivyotuagiza Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hizi ili nchi iende mbele.

"Jukumu letu la kwanza ni kuhakikisha kujua mradi huu umekwama wapi na tunakwendaje mbele kuanzia hapo. Na mradi huu tumeuona na thamani ya fedha inaonekana, kwangu mimi binafsi nimeridhika sana. Jambo la msingi pale ambapo tumepeana maelekezo katika kikao juu ya kutafuta zile funds (fedha) kwa ajili ya kukamilisha mradi huu, nadhani sasa twende tukahakikishe zinapatikana.

"Wale partners wetu ambao wanakwenda kusaidia tuhakikishe kwamba tunafanya nao mawasiliano haraka iwezekanavyo na mimi kwa upande wangu kama Naibu Waziri nikuhakikishie kwamba nitakupa ushirikiano mkubwa sana tuhakikishe kwamba mradi huu unakamilika na mambo yanakwenda kuwa mazuri kabisa kwa Watanzania,"amesema Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete. 

Amesema kuwa, mradi huo umefikia asilimia 93 ukiwa umekaribia kukamilika, hivyo kipande ambacho kimebakia ndicho wanatafuta fedha ili kukikamilisha na kati ya mwezi wa sita au wa nane jengo hilo la kisasa litakuwa linaanza kutumika.

"Mradi huu umefikia asilimia 93 na tayari tumeshaomba fedha, hivyo tunasubiri sasa wenzetu wa Wizara ya Fedha (Wizara ya Fedha na Mipango) kuweza kutupatia fedha iliyosalia kiasi cha shilingi bilioni 25.7 kwa ajili ya kukamilisha mradi huu,"amesema Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.

Uongozi NHC

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt. Maulid Banyani amesema, mradi huo gharama halisi zilikuwa ni shilingi bilioni 137.5 za kimkataba, zimetumika shilingi bilioni 112.4 na mpaka kukamilika kwa mradi zinahitajika shilingi bilioni 25.7 na tayari wameshapata ridhaa ya kupata fedha hizo.

"Kwa hiyo sasa tunaendelea taratibu na wadau wenzetu ili kukamilisha mchakato wa kupata fedha zilizobaki kwa ajili ya kukamilisha mradi huu ambao tunatarajia ndani ya miezi sita kukamilika,"amesema Dkt.Banyani.

Amesema, mradi huo umegawanyika katika maeneo manne ambapo eneo la kwanza ni kwa ajili ya hoteli ambayo ina vyumba 81 huku baadhi ya watu wakiwa wameonyesha utayari wa kununua na wengine kupangisha.

Pia amesema kuwa, mradi huo ukikamilika utatoa fursa nyingi za ajira kutokana na uwekezaji wa shughuli za biashara zinazofanyika kwenye majengo hayo.

"Ni hoteli ambayo ni self contained, itakuwa na vyumba ambavyo unaweza kujipikia na kufanya vitu vingine. Eneo la pili ni kwa ajili ya makazi, kuna takribani nyumba 40 ambazo zimekwisha nunuliwa, zimebaki nyumba sitini, matarajio yetu ni kuuza nyumba ishirini za ziada, zitakazobaki tutakuwa tunapangisha, tukipangisha kodi tutasema wakati mwingine ukifika.Lakini yatakuwa katika bei za kawaida.

"Eneo la tatu ni kwa ajili ya maduka, maeneo ya sinema ambapo kutakuwa na kumbi mbili za sinema. Kutakuwa pia na maeneo kwa ajili ya chakula na maeneo ya biashara ndogondogo na eneo lililobaki kwa ajili ya ofisi mbalimbali,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Taifa la Nyumba (NHC),Dkt.Sophia Kongera alishukuru ujio wa Naibu Waziri ambapo ameshuhudia kazi ikiendelea na wanatarajia fedha zilizobaki zitapatikana mapema ili muda wowote mradi huo ukamilike kwa ajili ya kutoa huduma. 

Heshima ya NHC

Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) ni kati ya mashirika ya umma yaliyojijengea heshima kubwa nchini kutokana na namna ambavyo linatekeleza miradi yake kwa viwango na ubora wa Kimataifa.

Morocco Square ni kati ya miradi minne mikubwa ya shirika hilo ambayo inaendelea kutekelezwa ukiwemo wa Kawe 711, Golden Premier Residence (GPR) na Plot (Kitalu) 300 Regent Estate jijini Dar es Salaam.

Mbali na miradi yao wenyewe ambayo wamekuwa wakiitekeleza sehemu mbalimbali nchini, NHC pia walipewa miradi mbalimbali ya kimkakati na Serikali ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo jumla ya miradi 17 yenye majengo 44 ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 12.96 ilitekelezwa mwaka jana.

Pia, NHC imejenga majengo ya ofisi ikiwemo ya Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kwa shilingi bilioni moja, ofisi za halmashauri za Malinyi mkoani Morogoro kwa shilingi bilioni 3.78 na Wanging'ombe mkoani Njombe kwa shilingi bilioni 2.7.

Aidha, pamoja na miradi hiyo Serikali ililipatia shirika kandarasi ya kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusingi Mitengo mkoani Mtwara kwa shilingi bilioni 15.8, Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kwangwa mkoani Mara kwa shilingi bilioni 17.2 na machinjio ya kisasa ya Vingunguti mkoani Dar es Salaam kwa shilingi bilioni 15.2.

NHC pia wameweza kuimarisha maeneo ya mipaka yetu kwa kujenga majengo makubwa ya biashara likiwemo jengo la Mutukula Commercial Complex walilolijenga katika mpaka wa Tanzania na Uganda na sasa wapo katika mpango wa kujenga jengo kubwa la biashara katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Kirongwe mkoani Mara. Hiyo ni baadhi ya miradi michache kati ya mingi ambayo imetekelezwa na NHC kwa ufanisi mkubwa,na inaendelea kutoa huduma kwa wananchi mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments