SIMULIZI JADIDA KUTOKA CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

SIKU moja siikumbuki tarehe, lakini ilikuwa mwaka 2013 mkoani Manyara katika kikao na wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkoani hapo tulileta ajenda ya ujenzi wa ukumbi wa Mitihani katika eneo letu lililopo Bagara Miyomboni Babati Manyara lipatalo ekari 24.
Katika kikao hicho kulikuwa na ajenda kadhaa na ilipofika ajenda ya Ujenzi, Mkurugenzi wa kituo Mr. Kassim Salehe Kimweri wakati huo alinipatia jukumu la kuelezea ajenda hiyo mimi Mohamed Omary Maguo wakati huo bado sijawa daktari bali Mhadhiri msaidizi.

Hakika ilikuwa ni fursa adhimu na niliitumia vizuri kuwaeleza wanafunzi juu ya ujenzi wa ukumbi wetu wa mitihani kwenye eneo letu.

Kwanza nilianza kwa kuwaeleza wanafunzi umuhimu wa kujenga eneo letu kwani ilikuwa tunakodisha ukumbi wa Mitihani kwa kiasi cha Shilingi za Kitanzania 3,000,000 kwa kila kipindi cha mitihani kwa wiki tatu.

Kwa mwaka tulikuwa na vipindi viwili vya Mitihani na kufanya kiasi cha Shilingi 6,000,000.

Hivyo nikawaambia kwamba inawezekana kabisa sisi tukajenga ukumbi wetu na hizi fedha za chuo za kulipa kila kipindi cha mitihani tukaziokoa zikafanya mambo mengine.

Nikawaambia wanafunzi, mnakumbuka tulipoanza kukodi ukumbi huu kwa ajili ya mitihani ulikuwa umeezekwa bati tu hata madirisha hayakuwepo...

Lakini leo ukumbi safi kabisa...maana yake fedha zetu ziwewezesha finishingi ya ukumbi huu...wakasema ndiyo... Naam twaibu... 

Nikiyasema maneno haya mmiliki wa ukumbi yupo kwa sababu alikuwa ni mjumbe wetu wa kamati ya ushauri ya mkoa ya Chuo almaarufu RAC.

Hata hivyo aliona ni jambo jema ila alikuwa na uhakika litachukuwa muda mrefu mpaka kukamilika kwake hivyo ataendelea kufaidi...

Baada ya maelezo hayo nikawauliza wanafunzi mnasemaje... Wakasema tupo tayari kujenga ila sasa hatujajua tutajenga vipi kwa fedha kutoka wapi?.

Nikawaambia sikilizeni... Wangapi hapa wamewahi kuchangia harusi... Kama unavyojua wanafunzi wetu wengi ni wafanyakazi na hivyo wote walinyoosha mkono kama ishara kuwa wamechangia harusi nyingi sana. 

Naam... Tumechanga Sana... Zikisikika sauti kutoka kila kona ya ukumbi.

Nikawaambia sasa uongozi wa kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania chini ya DRC Mr. Kassim Salehe Kimweri na uongozi wa OUTSO yaani Serikali ya Wanachuo Manyara Rais akiwa ndugu Pasian Siay tumekuja na mapendekezo.... 

Ni yapi hayo... Sauti zilisikika zikiuliza... Mapendekezo hayo ni kwamba kila mwanafunzi wa kituo chetu cha Manyara bila kujali anasoma ngazi gani atachanga kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi 20,000 kwa mwaka kwa ajili ya kuanza kuandaa fedha za ujenzi.

Tutachanga hivyo mpaka tufikishe kiwango fulani ndipo sasa tuiombe Menejimenti ya Chuo Makao Makuu tuitishe harambee kubwa na katika harambee hiyo tuwaeleze sisi tayari tuna hiki hivyo tunawaomba mtuchangie tujenge ukumbi wa mitihani kwenye eneo letu.

Baada ya pendekezo hilo... Ukumbi ulilipuka kwa shangwe... na kusema tupo tayari kuchanga. Basi wanafunzi wote waliandika majina na kuweka sahihi zao kama ishara kuwa agenda hiyo imeungwa mkono mia kwa mia.

Hapo hapo nikawageukia na kuwaambia kama mmekubali basi tuanze kuonesha mfano tufanye harambee hapahapa ya harakaharaka.... Pesa zilichangwa na ahadi zikatolewa... Kazi ikaanza.

Ukusanyaji wa fedha uliendelea vizuri sana mpaka ilipofika mwaka 2017 tayari kwenye akaunti kulikuwa na kiasi cha Shilingi Milioni 20. Mheshimiwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Kayanza Peter Pinda alifanya ziara ya kutembelea kituo cha Manyara mwaka 2018.

Katika risala yao wanafunzi walieleza kwamba wamekuwa wakichanga elfu 20 kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa mitihani na sasa zipo Milioni 20 kwenye akaunti...

Kimsingi akaunti hii ilikuwa ni ya OUTSO Manyara na mpaka leo ipo na fedha zinaendelea kukusanywa. Wasimamizi wa akaunti hiyo ni OUTSO kwa upande mmoja na Mkurugenzi wa kituo kwa upande wa pili...

Hivyo pesa haipotei hata senti moja. Wakileta maombi ya kutoa pesa zao... Mkurugenzi wa kituo kabla ya kusaini cheki aliniita ili nimwambie balansi ya fedha za ujenzi ni kiasi gani na za OUTSO ni kiasi gani....

Kama walishatumia fedha zao zikaisha kamwe hatukuwaruhusu kugusa hata senti moja ya fedha za ujenzi.

Basi Mheshimiwa Mkuu wa Chuo alifurahishwa sana kusikia wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkoa wa Manyara wamechanga kiasi hicho cha fedha....

Akasema "Hakika mmefanya jambo kubwa mno sikutarajia... Mara nyingi tumekuwa tukisikia wanafunzi wanagoma wanataka fedha ninyi mnatoa fedha kiasi hicho kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa mitihani... 

Sijatarajia... Sasa nawaahidi kuwa ombi lenu la kufanya harambee kubwa nimeafiki na nitasimamia harambee hiyo mapema iwezekanavyo. Kweli mwezi Oktoba 2018 ilifanyika harambee kubwa ikapatikana Jumla ya fedha za Kitanzania Milioni 150.

Kazi ya ujenzi ikaanza mara moja na tukiwa katika hatua ya msingi... Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano vya Mikoa ya Manyara, Geita, Kigoma, Lindi na Simiyu. Vituo vyote vimekamilika na vimeanza kutumika.

Si ukumbi wa mitihani tu bali pia kuna ofisi za walimu, maktaba, maabara ya Compyuta, ofisi ya OUTSO, vyumba vya kujisomea, vyumba vya kufanyia mijadala...katika mikoa tajwa.

Hakika ni shukurani ya pekee kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kufanikisha haya.

Pia, shukurani za dhati kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Mkoa wa Manyara kwa moyo wao wa maendeleo na tunawasihi waendelee na iwe pia ni chachu kwa vituo vingine vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuiga mfano huu.

Hata kama tayari kituo kina majengo bado kuna mengi mnaweza kufanya kwa michango ya aina hii yenye tija kwa vizazi na vizazi... Mchango wa OUTSO umesaidia sana kwani kituo kina ukumbi mkubwa unaoweza kuchukuwa watu takribani 1000 kwa wakati mmoja.

Wakati ule niliwaambia wanafunzi kwamba tunaanzisha mchango huu lakini huenda ukumbi ukikamilika tutakuwa hatupo Manyara tukawa sehemu nyingine na ndivyo ilivyotokea...

Mimi nipo Makao Makuu Dar es Salaam na wapo wanafunzi wengi na wafanyakazi wa chuo wengine wamehama lakini majengo yanawanufaisha Watanzania waliopo mkoani hapo kwa sasa. Pia, niongeze kuwa mchango ulikuwa unahusisha wafanyakazi wa chuo pamoja na wanafunzi. 

Kwa dhati kabisa napenda kumpongeza Mkurugenzi mwanzilishi wa kituo cha Mkoa wa Manyara cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dr. Asantiel Makundi wakati haya yote tunafanya yeye ndiye alikuwa akishauri hatua kwa hatua.

Ni mstaafu kwa sasa lakini bado ni hazina kubwa kwa chuo chetu... Na pia ni mtu aliyetufundisha kazi mpaka leo tupo hapa tulipofika.

Pia, pongezi za dhati zimfikie Dr. Joseph Magali kwa Sasa ni Mkuu wa Kitivo cha Biashara lakini naye alimpokea Mr. Kassim ukurugenzi na akayasimamia yote haya mpaka leo tunashuhudia mafanikio makubwa.

Shukurani za dhati zimfikie Mhe. Alexander Mnyeti aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa mchango wake mkubwa katika kusimamia ujenzi na kutoa uongozi stahiki.

Harambee ya ujenzi tuliyofanya ni yeye ndiye alikuwa mwenyeji na msimamizi na ndiye aliyetoa mwaliko kwa wanaharambee wote waliohudhuria.

Tunamshukuru sana, wakati fulani kati kati ya ujenzi aliwezesha kupatikana kwa vifusi bila malipo yoyote kutoka chuoni bali kutoka kwa wahisani na wadau wa maendeleo.

Pamoja nae tunawashukuru viongozi wote wa Mkoa wa Manyara wa sasa na wale waliokuwepo wakati huo. Wabarikiwe sana kwa mchango wao mkubwa.

Kwa uongozi na Menejimenti ya Chuo kwa kweli ndio waliotoa miongozo na baraka zote mpaka mafanikio haya yanatokea. Profesa Tolly Mbwette Mungu amrehemu, Profesa Elifas Tozo Bisanda ndiye aliyesimamia ujenzi wote akisaidiwa na Prof. Deus Ngaruko Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. George Oreku Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Rasilimali na Prof. Alex Makulilo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Huduma za Mikoa na Taalima za Kujifunzia. Tunawashukuru sana kwa kazi nzuri.

Nimeamua kutoa simulizi hii ili kutoa hamasa kwa wanafunzi, vijana na Watanzania kwa ujumla tuwe wazalendo kwa nchi yetu kwa kujitolea kadri tuwezavyo. Ukisoma simulizi hii kuna mengi ya kujifunza sana na tunaweza kushea na wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo na vyuo Vikuu.

Mwandishi

Dkt. Mohamed Omary Maguo 

Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Post a Comment

0 Comments