Watumishi Bunda mguu ndani, mguu nje, RC Hapi aibua madudu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI mkoani Mara imewasilisha maombi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ili kutengua baadhi ya Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambao wameonekana kutozitendea haki nafasi zao kwa kutowajibika ipasavyo.
Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kijiridhisha kuwepo ubinafsi na uzembe wa hali ya juu katika usimamizi wa miradi katika halmashauri hiyo.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Isanju katika halmashauri hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema baadhi ya wakuu wa idara katika halmashauri hiyo, wamekuwa ni kikwazo katika utekelezaji wa miradi licha ya Serikali kutoa fedha.
Hapi amezitaja idara hizo kuwa ni Idara ya Manunuzi, Mipango na Fedha, ambapo kwa pamoja idara hizo zimesababisha kusuasua kwa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Isanju licha ya Serikali kutoa fedha tangu mwezi Septemba,mwaka jana.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho, fundi anayetekeleza mradi huo, Robert Mwijarubi amesema ujenzi umesimama kutokana na kukosewa kwa vifaa ambavyo awali vililetwa lakini ikabainika kuwa vifaa hivyo sio sahihi.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari amesema halmashauri hiyo imekuwa na shida kwenye utekelezaji wa miradi na kusema kuwa watumishi hao wamekuwa na tabia ya kujinufaisha binafsi huku miradi ikishindwa kutekelezwa.

Post a Comment

0 Comments