Ajinyonga kwa kamba ndani ya chumba cha mpenzi wake

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKAZI wa Kitongoji cha Mpanda Hoteli Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi,Willy Mwakapimba (48) amejinyonga kwa kutumia kamba kwenye chumba cha mpenzi wake aitwaye Hawa Ayubu na kuacha ujumbe ulioandikwa kuwa, alisikia sauti ya marehemu mama yake ikimtaka aende akafukue kaburi ili atoe vitu vya kishirikina.

Michael Sikenyenzi ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kivukoni Kata ya Shanwe amesema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4:15 huko Kata ya Shanwe Manispaa ya Mpanda.

Amesema, tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya marehemu kutoka Kituo cha Polisi cha wilaya alikokuwa amekwenda kuripoti baada ya kushikiliwa kwa kosa la kufukua kaburi.

Sikenyenzi amesema kuwa, alipigiwa simu na kuitwa nyumbani kwa Hawa na alipofika alikuta marehemu akiwa amejinyonga chumbani, hali ambayo ilimlazimu atoe taarifa polisi ambapo walifika kwenye eneo hilo.

Amesema kuwa, kwenye chumba hicho walikuta ujembe wa maandishi aliokuwa ameandika marehemu ukieleza kuwa alisikia sauti ya marehemu mama yake ikimtaka aende kwenye kaburi lake akafukue, kwani kuna vitu vimefukiwa na ndugu yake ambaye amekuwa akiwafanyia vitendo vya kishirikina ndugu zake.

Mwenyekiti huyo alisema, baada ya kusoma ujumbe huo aliwahoji ndugu wa marehemu waliokuwa wamefika kwenye eneo hilo akiwemo kaka mkubwa wa marehemu ambaye alidai kuwa ni kweli mdogo wake alikwenda kwenye makaburi ya Mwangaza na kufukua kwenye kaburi la mama yao na kukuta kichwa kinachosadikiwa ni cha binadamu na sehemu ya siri ya mwanamke, sanda na kitambaa chekundu ambavyo alivichukuwa na kuvipeleka dukani kwa ndugu yake aliyekuwa akimtuhumu kuwa ni mshirikina.

Alieleza kuwa, baada ya kuwa amevipeleka vitu hivyo Februari 11,2022 kwenye duka hilo lililopo kwenye Mtaa wa Mpanda Hoteli polisi walipata taarifa ya kuwa kumetokea kitendo hicho na walimkamata marehemu huyo na kumuweka mahabusu hadi siku iliyofuata mchana.

Mke wa marehemu huyo, Hawa Ayubu alisema kuwa, yeye na marehemu walikuwa wakiishi kama mume na mke kwenye nyumba ambayo aliachiwa na mume wake ambaye alifariki dunia na kumwachia nyumba hiyo ambapo kwenye maisha yake na Willy wamefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike.

Amesema kuwa, yeye alipigiwa simu na mume wake huyo ambaye alimtaka awahi kurudi nyumbani kwani alikuwa na shida naye ndipo alipofika nyumbani na alipoingia ndani ya chumba walichokuwa wanalala alimuona mumewe akiwa amejinyonga juu ya paa la nyumba kwa kutumia kamba huku pembeni kukiwa na stuli jirani na kitanda.

Mmoja wa majirani Anasitazia John alisema kuwa walisikia mayowe ya Hawa Ayubu akipiga kelele ya kuomba msaada hali ambayo iliwalazimu wao majirani wafike kwenye eneo hilo na walipofika ndani ya chumba walikuta mwili wa marehemu ukiwa juu ya paa ya nyumba huku akiwa amejinyonga na mkewe Hawa akiwa amepoteza fahamu kutokana na mshituko wa kifo cha mume wake.

Post a Comment

0 Comments