Benki Kuu yataja faida za kusajili vikundi vya kijamii vinavyokopeshana fedha nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania imesema kuwa, faida za jamii kusajili vikundi vya kuweka na kukopeshana fedha katika maeneo mbalimbali nchini ni nyingi zaidi ya hasara ambazo zinazoweza kupatikana wakiwa wanasimamia vikundi vyao kienyeji.
Hayo yamebainishwa Februari 15, 2022 na Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Usimamizi wa Idara ndogo za Fedha pamoja na Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani katika siku ya pili ya mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara yanayoendelea katika Ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mbeya.

Katika mafunzo hayo ya siku tano ambayo yanaratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Mnyamani alikuwa anawasilisha mada ya mafanikio na changamoto tangu kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na kanuni zake.

Pia changamoto za usimamizi wa watoa huduma ndogo za kifedha na kanuni za kumlinda mlaji wa huduma za fedha (financial consumer protection).

"Kuna faida nyingi sana za hivyo vikundi kujisajili na kutambulika rasmi, kwanza mbali na kutambulika usalama wa fedha za wanachama unakuwa mkubwa zaidi kuliko mtu mmoja kubebeshwa jukumu la kutunza fedha zote nyumbani.

"Kama hamtambuliki, hamna mfumo rasmi wa kukiendesha kikundi chenu na mnaendesha shughuli za kuweka na kukopeshana fedha, siku linaweza kutokea la kutokea yule ambaye mlimuamini akawa anawatunzia fedha zenu mfano kwenye akaunti yake ya benki, ikatokea akafariki na amekusanya fedha nyingi,mtakwenda kuanzia kudai kwa nani?

"Ile akaunti si itakuwa chini ya familia yake, sasa unafikiri hao wanafamilia watakubaliana na ninyi ambao mlimuamini aliyefariki. Nichukue nafasi hii kuwashauri wote ambao wamejiunga katika vikundi ambavyo havijasajiliwa, na wanaendelea kuweka na kukopeshana fedha wakajisajili ili kupata faida zaidi,"amefafanua.

Bw.Mnyamani ametaja vitu vya msingi akiangazia Kanuni za Watoa Huduma Ndogo za Fedha (Vikundi vya Kijamii) Kanuni za mwaka 2019 ambazo zinajumuisha masharti ya Uanzishaji wa Kikundi (Kanuni za 4-7).

"Kuna mkutano wa awali,kamati ya mpito na majukumu yake na kikao cha uanzishaji na majukumu yake. Masharti ya Usajili wa Kikundi (Kanuni za 8-17) yanataka maombi ya usajili yawasilishwe Mamlaka Kasimishwa na yaambatane na nakala ya katiba yenye sahihi za wanachama, nakala za mihtasari ya mkutano wa uanzishaji, maazimio ya wanachama kuanzisha kikundi, mapendekezo ya muundo wa kikundi, uthibitisho wa malipo ya michango ya awali, barua ya mamlaka ya kata au kijiji;

"Jina la kikundi lijumuishe maneno 'Kikundi cha Huduma Ndogo za Fedha cha Kijamii'. Maombi kuchakatwa katika kipindi cha siku 14 na kikao cha kwanza kufanyika ndani ya mwezi mmoja,"amefafanua Bw.Mnyamani.

Bw.Mnyamani amesema kuwa, Bunge la Jamhuri lilipitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mnamo tarehe 23 Novemba mwaka 2018 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017 ambayo pamoja na mambo mengine ilibainisha umuhimu wa kuwepo kwa Sheria na Kanuni ili kudhibiti mapungufu katika sekta husika.

"Madhumuni makubwa ya sheria ni kutoa mamlaka ya kusajili,kutunga kanuni na kusimamia biashara ya huduma ndogo za fedha na masuala mengine na sheria hii inatumika Tanzania Bara peke yake,"amesema Bw.Mnyamani.

Ameendelea kufafanua kuwa, sekta ndogo ya fedha ni miongoni mwa sekta muhimu kwa wananchi wa kipato cha chini inayosaidia kuongeza kipato na kupunguza umasikini.

Pia inalenga kulinda watumiaji wa huduma ndogo za fedha, kuweza kupata taarifa au takwimu muhimu katika sekta ya fedha na uchumi kwa jumla.

"Na kuhakisha watoa huduma ndogo za fedha wanashiriki katika mfumo wa taarifa za mikopo ili kupunguza vihatarishi vya mikopo chechefu katika sekta ya fedha ikiwemo kuhakikisha utoaji wa elimu ya fedha kwa watumiaji wa huduma ndogo za fedha,"amesema Bw. Mnyamani.

Pia amesema, sheria imeweka watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja manne likiwemo daraja la kwanza ambalo ni benki zinazotoa huduma ndogo za fedha, pili taasisi zinazotoa mikpo bila kupokea amana za umma ikijumuisha kampuni za kukopesha, watoa huduma ndogo kwa njia za kidigitali na watu binafsi wanaokopesha.

"Tatu ni vyama vya ushirika vya akiba na mikopo kwa maana ya SACCOS na nne ni vikundi vya huduma ndogo za fedha vya kijamii kwa maana ya VICOBA, VSLAs na vinginevyo,"anafafanua Bw.Mnyamani.

Kwa mujibu wa Afisa huyo, sheria imebainisha kuwa benki zinazofanya biashara ya huduma ndogo za fedha zitasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Majukumu ya BoT ni yapi?

Bw.Mnyamani anasema kuwa, kwa mujibu wa sheria, majukumu ya Benki Kuu ni pamoja na kusimamia na kufuatilia watoa huduma ndogo za fedha.

Pia kutunga kanuni na kusimamia watoa huduma ndogo za fedha. "Benki Kuu inaweza kukasimisha mamlaka na majukumu yake kwa kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali.

"Kwa daraja la tatu, Benki Kuu inaweza kukasimisha mamlaka na majukumu yake kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), kwa daraja la nne, Benki Kuu inaweza kukasimisha mamlaka na majukumu yake kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Kwa daraja la pili isipokuwa kwa ruhusa ya Waziri, Benki Kuu haiwezi kukasimisha mamlaka na majukumu yake, kwani mamlaka kasimishwa itatekeleza mamlaka na majukumu yake kulingana na vigezo, taratibu na maelekezo ya Benki Kuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news