Rais Dkt.Mwinyi aendelea kusaka fursa kustawisha uchumi wa Zanzibar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameiomba AFREXIM Bank kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupata mchanganuo wa masoko wa zao la mwani, ili wakulima wa zao hilo hapa nchini waweze kunufaika kikamilifu.

Dkt.Mwinyi ametoa ombi hilo wakati alipokutana na Uongozi wa AFREXIM Bank kutoka nchini Misri, uliofika Ikulu jijini Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa mazungumzo yake na Serikali kwa lengo kubaini maeneo mbalimbali yenye fursa ya Uwekezaji hapa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Afrexim Bank kutoka nchini Misri ukiongozwa na Makamu wa Rais Mtendaji, Bw.Amr Kamel (kulia kwa Rais) wakipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo Februari 16,2022 (kushoto kwa Rais) ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaban na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu).

Amesema, kupitia Sekta ya Kilimo, Zanzibar inategemea mazao makuu mawili ya Biashara, ikiwemo zao la Mwani ambapo wakulima wa zao hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuuza mwani kwa bei ya kiwango cha chini katika masoko.

“Soko la zao la Karafuu liko vizuri, tatizo kubwa liko kwenye soko la zao la mwani, ni eneo ambalo tunahitaji kupata ushirikiano ili kuongeza kuliongezea thamani zao hilo pamoja na kuinua kiwango cha bei ili wakulima wetu waweze kunufaika,”amesema.

Dkt.Mwinyi amesema Zanzibar ina maeneo mengi ya uwekezaji kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu, ikihusisha sekta ya utalii, mafuta na gesi,uvuvi na kadhalika, hivyo akabainisha umuhimu wa benki hiyo katika kushirikiana na Serikali kuendeleza sekta hizo.

Amesema, Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya kuwa na miundombinu chakavu isiyokidhi mahitaji ya uhifadhi wa mafuta.

Rais Dkt.Mwinyi amepongeza utayari wa benki hiyo katika kuendeleza mazungumzo yatakayofanikisha kuanzishwa kwa ujenzi wa miundo mbinu ya Kituo cha mikutano ya Kimataifa pamoja na maeneo ya viwanda.

Ameipongeza Benki ya AFREXIM kwani ina uwezo mkubwa na imekuwa ikishirikiana na Serikali mbalimbali Barani Afrika katika uwekezaji wa miradi mkubwa ya maendeleo.

Aidha, alipongeza juhudi za uongozi wa benki hiyo wa kukutana na Uongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kwa lengo la kujadili fursa mbalimbali zilizopo nchini, ambapo AFRIMEX Bank inaweza kusaidia katika nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa mikopo kwa Mmkampuni mbalimbali.

Nae, Makamu wa Rais Mtendaji, Maendeleo ya Biashara na Benki ya Ushirika ya AFREXIM Bank, Amri Kamel alimpongeza mapokezi makubwa waliyopata, sambamba na kupata fursa ya kuona maeneo mbalimbali ya uwekezaji.

Aidha, alisema uongozi huo utaendelea kuzungumza na taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta za uwekezaji pamoja na kufanyia kazi ushauri uliotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ili kufanikisha malengo yaliokusudiwa.

Ujio wa Uongozi wa AFREXIM Bank hapa nchini unafuatia ziara iliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi , mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini na kukutana kwa mazungumzo na uongozi wa benki hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news