RC Kafulila asitisha wasambazaji malighafi ujenzi chuo cha VETA Simiyu

NA DERICK MILTON

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila ameagiza kusitishwa mara moja matumizi ya wakandarasi ambao wamepewa kazi za usambazaji wa vifaa vya ujenzi katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA mkoani humo ambao si wakazi wa mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafila akipitia nyaraka za ujenzi wa Chuo cha VETA mkoani humo, ambao unasimamiwa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunhamala Bariadi.

Hatua hiyo ya Mkuu wa Mkoa imekuja baada ya kutembelea mradi huo akiwa na Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa na kupewa maelezo ya mmoja wa wakandarasi wa kusambaza tofali kuwa anatoka Mkoani Mwanza.

Baada ya kupata maelezo hayo, Mkuu huyo wa Mkoa akaagiza mkandarasi huyo ambaye ni Arm Strong Company Ltd kusitishiwa mkataba wake na badala yake anafutwe msambazaji mwingine ambaye ni mkazi wa mkoa wa Simiyu.

Alisema kuwa siyo sahihi mkoa wa Simiyu kuwa hauna watu wenye uwezo wa kusambazaja baadhi ya malighafi za ujenzi, ambapo alitolea mfano taasisi kama Magereza na baadhi ya wafanyabishara wa mkoa wa Simiyu ambao wamekuwa wakifanya kazi hizo.

Alisema kuwa hataki kuona mtu yeyote kutoka nje ya mkoa wa Simiyu akifanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na watu wa mkoa wake na badala yake kuwepo na maelekezo maalumu ambayo ni kataalamu.

“ Ni marufuku kutumia watu kutoka nje ya mkoa, na yule ambaye anasambaza tofali kuanzia sasa asimame, atafutwe mtu mwingine wa mkoa wa Simiyu, zibaki kazi zile ambazo wakazi wa mkoa wa simiyu hawawezi,” alisema Kafulila.

“ Kwa mfano kuna wanao sambaza nondo, saruji kama ni kiwanda chenyewe hiyo sawa, lakini kama ni mtu basi atoke hapa Simiyu na siyo kutoka katika mkoa mwingine,” aliongeza Kafulila.

Amesema kuwa wakandarasi ambao wamepewa kazi hiyo ya kusambaza vifaa vya ujenzi katika mradi huo kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa wa mkoa wa Simiyu, mikataba yao isitishwe mara moja na wabaki wale ambao malighafi hazipatikani ndani ya mkoa.

Katika hatua nyingine Kafulila aliagiza kufanyiwa marekebisho makubwa kamati ya ujenzi, baada ya kubaini wanaounda kamati hiyo ni wachache lakini pia hawana utalaamu na mambo ya ujenzi.

“ Kamati hii ya ujezi ifanyiwe marekebisho makubwa, waletwe watu ambao wanafahamu mambo ya ujenzi (wataalamu) huu mradi ni mkubwa sana, kwanza hawa ni walimu, wanatakiwa kufundisha chuoni huku wasimamie ujenzi hawawezi,” alisema Kafulila.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhnamala, Bazil Ngoloka ambao ndiyo wasimamizi wa ujenzi huo amesema kuwa serikali imetoa kiasi cha sh. Bilioni 5.1 kwa ajili ya kujenga chuo hicho.

Ngoloka alisema kuwa ujenzi huo umeanza mwezi Februari na mkataba wa ujenzi ni miezi sita, ambapo mpaka sasa wamelipa kiasi cha shilingi Milioni 789 zimelipwa kwa ajili ya kununua malighafi na mafundi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange akawalalamika Wizara ya Elimu kwa kuleta miradi kwenye Wilaya yake ukiwemo ujenzi huo wa chuo cha VETA bila ya kushirikisha ofisi yake na kutafuta wakandarasi kutoka nje ya Wilaya na Mkoa.

Post a Comment

0 Comments