Serikali yadhamiria kufufua Bandari ya Musoma

NA FRESHA KINASA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, Serikali yake imedhamiria kufufua Bandari ya Musoma ianze kufanya kazi ili kuwezesha usafiri wa meli katika kuufungua uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla. 
Muonekano wa mji wa Musoma. (Picha na Mtandao).

Ameongeza kuwa,  nia ya Serikali ni kuona mkoa unapiga hatua kimaendeleo na ndio maana imeendelea kuimarisha miundombinu ya barabara na Uwanja wa Ndege wa Musoma. 

Ameyasema hayo leo Februari 7, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa Butiama katika ziara yake ya kiserikali mkoani humo, ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa maendeleo yanayofanywa ni matokeo ya uongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuanzia awamu ya kwanza hadi sasa.

Pia, Mheshimiwa Rais amewahimiza wakazi wa Butiama na Watanzania kwa ujumla, kufanya kazi kwa bidii huku akibainisha kwamba Serikali itaendelea kutatua changamoto maeneo mbalimbali kwa masilahi mapana ya Watanzania.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa, kupitia mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari- Butiama utasaidia kumaliza changamoto ya maji pamoja na ufungaji wa pampu ulioanza kufungwa hivi karibuni utasaidia kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa Butiama.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kayegele amesema anaishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa 72, na shule shikizi vyumba vyumba sita. 

Naye Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti upande wa TARURA Mkoa wa Mara kutoka Shingi Bil.9.7 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Shilingi Bil.25.4 kwa mwaka 2021/2022 ili kuboresha barabara.

Pia, Bashungwa amewahimiza wazazi na walezi mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla, kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanakwenda shule kwani serikali imekuwa ikigharimia mpango wa elimu bila malipo kuwezesha wote wasome.

Post a Comment

0 Comments