TANESCO kuja kivingine kuanzia Aprili mwaka huu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema moja ya mkakati wake ni kwamba kuanzia Aprili, mwaka huu linataka mteja anapoomba kuunganishiwa umeme basi aunganishiwe ndani ya siku saba na isiwe zaidi ya siku hizo huku likitoa rai kwa wananchi wasikubali kutoa rushwa kwa namna yoyote ile kwa lengo la kupatiwa huduma.
Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini wakiendelea na kazi ya kuunganisha umeme katika nyumba ya moja ya wateja wao ambao wamelipia sh.27,000 katika Mtaa wa Matosa,King'ong'o na Kimara B.
 
Hayo yamesemwa leo Februari 20, 2022 na Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Martin Mwambene wakati akizungumzia kuhusu utekelezaji wa kampeni ya Shirika hilo ya kuunganisha umeme kwa wateja wote ambao wamelipia sh.27,000 inayoendelea nchini kote ambayo imeanza rasmi jana.

"Leo ni muendelezo wa kampeni ambayo tumeianzisha na tuko hapa Kinondoni Kusini ambako ni miongoni mwa mikoa 129 na Wilaya 132 ambazo TANESCO tunazo nchi nzima, tunalofanya hapa ni kuhakikisha wateja waliofanya malipo ya Sh.27,000 wanaunganishiwa umeme na jana tulisema tulikuwa na wateja 90,000 na wanaendelea kupungua.

"Lakini lengo la hii kampeni tunataka sasa mteja awe ana unganishiwa umeme ndani ya siku chache zaidi, tunataka iwe chini ya siku saba na isizidi siku hizo.TANESCO malengo yetu ni kuona mteja akiomba tu umeme basi anaunganishiwa ikiwezekana ndani ya siku moja, mbili au tatu na ikiwa imeshindikana kabisa isizidi siku saba,"amesisitiza Mwambene.

Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Martin Mwambene akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 20,2022 kuhusu kampeni ya kuunganisha umeme inayoendelea nchini kote ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza moja ya malengo yao kuanzia Aprili, mwaka huu mwananchi akiomba umeme basi ndani ya siku saba awe ameunganishiwa umeme.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi wote hasa ambao ni wateja wa TANESCO wakiwemo walioomba kuunganishiwa umeme wasikubali kutoa fedha yoyote ile kama fedha ya ziada ili kuunganishiwa umeme au kupata huduma za Shirika.
 
"Mwananchi ukishalipa fedha ya kuunganishiwa umeme iwe Sh.27000 au fedha yoyote ile ambayo utakuwa umelipa kwa kutumia namba ya malipo, hutakiwi kutoa fedha yoyote ili kupata huduma zetu,"amesema.
Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini wakipitia nyaraka muhimu za moja ya wateja ambao wako katika orodha ya wanaostahili kuunganishiwa umeme katika mtaa wa Matosa.

Ameongeza, haijalishi mteja atakuwa mbali kiasi gani au alikuwa anataka nguzo ngapi, gharama ikishalipwa kwa utaratibu unaoeleweka kupitia namba ya malipo hakuna malipo ya ziada na kusisitiza malipo yote yanayohusu TANESCO yanalipwa kwa 'Control Number' na sio vinginevyo kwani nje ya hapo itakuwa ni rushwa.
"Hivyo nitoe rai usitoe rushwa na usishawishike kutoa rushwa".
Wananchi wakifuatilia maelezo ya Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Martin Mwambene (hayupo pichani) kuhusu mipango mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo katika kuwahudumia wananchi.

Awali Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Mhandishi Nickson Babu akizungumza kampeni ya kuunganishia umeme wateja waliolipa Sh.27000 amesema kwa leo wanatarajia kuunganishia wateja 300 katika mitaa mitatu ya Matosa, King'ong'o na Kimara.Lengo ni kutekeleza utoaji wa huduma kwa wateja wao.

"Jumla ya wateja 4300 wamefanya malipo ya Sh.27000 na wote wanahitaji kupata huduma tena kwa wakati na sisi kama ofisi tumejipanga kuwahudumia na hao 300 tutakaouwanganishia wataanza kutumia umeme leo, kampeni hii ni endelevu mpaka pale wateja wote waliolipia wawe wameunganishwa na kabla ya kumalizika Machi tutauwa tumemaliza.
Zainabu Mohamed Hongo ambaye ni mkazi wa Matosa mkoani Dar es Salaam akiwasha taa kwa mara ya kwanza baada ya TANESCO Mkoa wa Kusini kumuunganishia umeme kwenye nyumba yake leo Februari 20,2022.

"Baada ya hapo tutaingia kwenye utaratibu mpya wa kuhakikisha mteja akiomba umeme anaunganishiwa ndani ya siku saba,"amesema.
 
Aidha. amewasisitiza wananchi wasikubali kutoa rushwa kwa lengo la kushawishi kupatiwa huduma kwa haraka bali wafuate utaratibu uliopo wa kulipa gharama zinazohitahika kwa kutumia namba ya malipo.
Watumishi wa TANESCO pamoja na wananchi wakiwa makini kufuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na viongozi wa TANESCO kuhusu utekelezaji wa kampeni ya kuunganisha umeme kwa wateja waliolipa sh.27,000.

"TANESCO gharama ambazo tunatoza ni ile ambazo tumeelekezwa na EWURA na zinalipiwa kwa Control number .Mteja akishapewa control number na akalipia hakuna kiasi chochote cha fedha ambacho mteja atatakiwa kulipa kama sehemu ya kuharakisha huduma yake, kitendo hicho kitatafsiriwa kama jinai kwa maana ya tendo la rushwa.

"Pamoja na sisi kutoa rai hiyo tumeamua kujipanga kwa kuharakisha utoaji huduma zetu kama nilivyosema , kwa hiyo tunavyoharakisha kutoa huduma maana yake tunakwenda kupunguza vitendo vya rushwa na vitakufa moja kwa moja,"amesema Mhandisi Babu.

Post a Comment

0 Comments