Uwekezaji katika Dhamana za Serikali unavyoweza kukuwezesha kuuaga umaskini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, kuna faida nyingi za kuwekeza katika Dhamana za Serikali ikiwemo viwango vya riba vinavyoridhisha.

BoT kwa niaba ya Serikali zote mbili huuza Dhamana za Serikali ikiwa ni njia ya kukopa fedha kutoka katika soko la ndani.

Dhamana za Serikali zimegawanyika katika makundi mawili ikiwemo Dhamana za Serikali za muda mfupi (Treasury bills),Dhamana za Serikali za muda mrefu (Treasury bonds).
Mchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Fidelis Mkatte ameyasema hayo leo Februari 15, 2022 wakati akiwasilisha mada ya Uwekezaji kwenye Dhamana za Serikali katika siku ya pili ya mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha.

Mafunzo ambayo yanaendelea katika Ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mbeya yakiratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania ambapo Bw. Mkatte amesema, katika kutekeleza jukumu hilo, Benki Kuu imekuwa ikiendesha minada ya dhamana za Serikali kulingana na mpango wa ukopaji (issuance plan) wa Serikali kutoka masoko ya mitaji ya ndani ya nchi, bila kuathiri mikopo kwa sekta binafsi.
"Kuna faida nyingi sana kwa wawekezaji kuwekeza katika Dhamana za Serikali. Mosi, kuwekeza katika Dhamana za Serikali ni salama kwani Serikali haitarajiwi kukiuka matarajio ya wadai wake wakati wa malipo.

"Pili dhamana za Serikali zinahamishika, hivyo mwekezaji anaweza kuziuza endapo itakuwa ni lazima kufanya hivyo. Tatu,Dhamana za Serikali zinaweza kutolewa kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo katika taasisi za fedha nchini. Pia Dhamana za Serikali zina viwango vya riba vinavyoridhisha,"amefafanua Bw.Mkatte.

Bw. Mkatte amefafanua kuwa,kupitia dhamana hizo, Serikali (mkopaji) huwa inapata fedha kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

"Pia huwa zinasainia katika kusimamia Ujazi wa Fedha katika Uchumi, hivyo kusaidia kusimamia mfumuko wa bei, kuchagiza Soko la Upili kwa kuuza Dhamana za Serikali katika Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) na kushirikisha wananchi katika ujenzi wa uchumi wa Taifa,"amebainisha.

Mchambuzi huyo wa Masuala ya Fedha ameendelea kufafanua kuwa,kupitia utaratibu huo kwa Masoko ya Fedha huhamasisha utafutaji wa mitaji kwa taasisi zingine.

"Kwa mfano Corporate Bonds, hutoa fursa za uwekezaji, kuwepo na ushindani katika uwekezaji mbalimbali hivyo kupatikana kwa riba za kisoko. Riba katika Dhamana za Serikali hutumiwa kama riba elekezi au anzio katika ukopaji na ukopeshaji mwingine.
"Kuwepo kwa Dhamana za Serikali, haswa za muda mrefu zinasaidia kukua kwa sekta zingine kama vile ukopeshaji kwa ajili ya ujenzi ama ununuzi wa nyumba (mortgages),"amebainisha Bw.Mkatte.

Nitashiriki vipi katika Dhamana za Serikali?

Bw. Mkatte anasema, mshiriki katika mnada Dhamana za Serikali anapaswa kufungua akaunti ya uwekezaji katika Benki Kuu kupitia kwa mawakala (CDP – Central Depository Participants) ambao ni mabenki yote pamoja na madalali (brokers) wa Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Anasema, ili kujiandikisha mtu binafsi anapaswa kuwa na nyaraka kama kitambulisho halali, kama leseni ya udereva, kitambulisho cha Taifa au cha mpiga kura,picha (passport size) ya rangi,TIN kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kodi.

Kwa upande wa vikundi mbalimbali, Bw.Mkatte amesema kuwa,ili viweze kukidhi vigezo vinapaswa kuwa na usajili wa kikundi na mahitaji mengine kama ya mtu binafsi.

"Ushiriki katika Dhamana za Serikali kwa upande wa watoto chini ya miaka 18 wanapaswa kuwa na cheti cha kuzaliwa cha mtoto, picha ya rangi ya mzazi au mlezi na mtoto, mahitaji mengine kama ya mtu binafsi.

"Baada ya mtoto kufikisha miaka 18 atatakiwa afanye yafuatayo, kuwa na uthibitisho wa umri,atafungua akaunti yake ya CDS, mahitaji mengine kama ya mtu binafsi,"amefafanua Bw.Mkatte.

Akizungumzia kwa upande wa mashirika au kampuni amesema zinapaswa kuwa na MERMATS,usajili wa kampuni,
leseni ya biashara, picha (passport size) za rangi za wakurugenzi na TIN kutoka TRA kwa ajili ya kodi.

Mchakato ulivyo

Bw.Mkatte amesema kuwa,akizungumzia kuhusu mchakato wa mnada na taratibu ya kutuma zabuni amesema, taarifa za kushiriki katika Minada ya Dhamana Serikali tangazo hutolewa kila Ijumaa katika gazeti la Serikali na kwenye
tovuti ya Benki Kuu.
"Mara baada ya matangazo, wawekezaji walio na akaunti za Dhamana za Serikali wanaweza kuwasilisha zabuni zao. Wawekezaji hujaza fomu za ushiriki, zinazopatikana katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania (http://www.bot.go.tz) au kupitia kwa mawakala wao na mawakala hujaza maelezo ya fomu za ushiriki kwenye mfumo wa CDS na kuziwasilisha Benki Kuu kielektroniki,"amesema Bw.Mkatte.

Bei ya Dhamana za Serikali

Bw. Mkatte anafafanua kuwa,bei ya Dhamana za Serikali utofautiana kwani, kila dhamana hutokana na nguvu ya soko kupitia minada.

"Dhamana za Serikali za muda mfupi zinauzwa kwa bei pungufu ya shilingi ya Kitanzania 100 (discount),dhamana za Serikali za muda mrefu zinauzwa ama kwa punguzo la mia (discount) au sawa na mia (Par) au zaidi ya mia (Premium).Bei zote za Dhamana za Serikali zinapaswa kuandikwa katika tarakimu nne za desimali,"amefafanua Mtaalamu huyo.

Matokeo

Bw.Mkatte akifafanua kuhusu matokeo ya mnada na taratibu za malipo anasema kuwa, matokeo ya minada hutolewa mara baada ya mnada husika kukamilika kupitia tovuti ya Benki Kuu na ofisi za mawakala (CDS Web Portal).

•"Malipo ya Dhamana za Serikali hufanyika siku moja baada ya mnada husika (Alhamisi),pia malipo hufanyika kupitia akaunti ya mteja iliyopo katika benki yake.

"Shilingi ya Tanzania tu ndio hukubalika kulipia dhamana za Serikali.Endapo mshiriki atashindwa kulipa, ushiriki wake utasimamishwa kwa muda wa mwezi mmoja,"ameongeza Bw.Mkatte.

Uuzaji na ununuzi upoje?

Kwa mujibu wa Mchambuzi huyo,mauzo na manunuzi ya dhamana za muda mfupi yatafanyika nje ya soko la hisa na ni kwa njia ya makubaliano kati ya muuzaji na mnunuzi (OTC-Over the Counter) na ni baada ya dhamana hizo kuuzwa katika soko la awali.

Bw.Mkatte amesema kuwa,dhamana za Serikali za Muda Mrefu zinasajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambapo muuzaji na mnunuzi wa Dhamana za Serikali, kila mmoja wao atawasilisha kwa wakala fomu za uhamishaji wa dhamana zilizojazwa sawia.
"Na fomu za uhamishaji wa Dhamana za Serikali zinapatikana katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania http://www.bot.go.tz,"amesema Bw.Mkatte.

Amesema kuwa, Benki Kuu inaendelea na uhamasishaji na elimu kwa umma wa watanzania wote kushiriki katika minada hii kama njia mojawapo ya kujiwekea akiba na kuchangia shughuli za uchumi na maendeleo ya nchi yetu.

Mifano ya Uwekezaji (Simulation)

Pia amesema, kupitia tovuti ya Benki Kuu, wameweka kikokotoleo (calculator) ambacho kinamuwezesha mwekezaji kufanya mahesabu na kuona anapata faida kiasi gani.
"Kikokotoleo hiki kinapatikana toka kwenye tovuti ya Benki Kuu kama ifuatavyo; Dhamana za Muda Mfupi (Treasury Bills): https://www.bot.go.tz/TBills/TbillsCalculator

"Dhamana za Muda Mrefu (Treasury Bonds): https://www.bot.go.tz/TBonds/TbondsCalculator ambapo anatoa angalizo kuwa, bei zilizopo kwenye kikokotoleo hicho, ni bei za wastani za minada iliyopita. Hivyo hubadilika kadiri minada mipya inavyofanyika,"amefafanua Bw.Mkatte.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news