Wadhamiria kufanya mageuzi uzalishaji wa mbegu za mazao

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MATUMIZI ya mbegu kama yatasimamiwa vyema itapelekea wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao yao ya kilimo.

Akizungumza na wadau wa kilimo wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Afisa Kilimo wa mkoa, Okrani Chengula amesema kuwa, uzalishaji wa mazao mengi na wenye tija unategemea pia matumizi ya mbegu sahihi.
Amedai kuwa, kutokana na umuhimu wa mbegu katika kilimo ipo haja ya kuunda jukwaa la wadau wa mbegu ambalo litakuwa na kazi kubwa ya kuhamasisha wakulima kupanda mbegu badala ya nafaka.

Afisa Kilimo huyo alidai kuwa, jukwaa hilo licha ya kuhamasisha jamii kupanda mbegu sahihi, lakini jukumu lao lingine litakuwa ni kushawishi wadau kuweza kuzalisha mbegu mkoani Rukwa badala ya kutegemea mbegu zinazozalishwa nje ya nchi.

Mchambuzi wa Sera kutoka SAGCOT, Prudence Lugendo alisema kuwa jukwaa la wadau wa mbegu kama litatumika vizuri linaweza kutengeneza ajenda na kuwa karibu na watafiti na kuweza kuzalisha mbegu wenyewe.

Alisema, jukwaa hilo litawashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha ambazo zinaweza kutoa hata mikopo kwa watu ambao watahitaji kuzalisha mbegu na kuacha kutegemea mbegu zinazozalishwa nje ya nchi na Tanzania kuwa dampo la begu zao wakati uwezo wa kuzalisha mbegu upo.

Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi, Pankrasi Maliyatabu alieleza umuhimu wa matumizi sahihi ya mbegu na kuwa kama matumizi ya mbegu yatakua ni makubwa kuna uwezekano mkubwa kwa wakulima kuweza kuzalisha mazao mbegu na kufanya mapinduzi makubwa katika sekta hiyo ya kilimo.

Hivyo alilitaka jukwaa la mbegu lililoundwa kufanya kazi inayostahili ili jamii ijue umuhimu wa matumizi ya mbegu na kuachana kupanda nafaka katika kuyafikia maendeleo halisi katika sekta hiyo ya kilimo.

Mkutano huo wa wadau wa mbegu ulifanikiwa kuunda jukwaa hilo la mbegu na kupata viongozi watakaloliongoza jukwaa hilo ambapo Richard Maganga alichaguliwa kuwa mwenyekiti,mwenyekiti mwenza ni Ladslaus Mzelela,Katibu Pirmin Matumizi,katibu msaidizi Musa Ng’wani na mtunza hazina Elia Siyame.

Post a Comment

0 Comments