Zijue athari tano zitokanazo na matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari

MARA nyingi watu wanaugua maradhi mbalimbali, lakini wengi wao hawapendi kwenda hospitali au kwenye vituo rasmi vya afya kufanya vipimo au kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa daktari.

Kutokana na uwepo wa maduka ya dawa baridi, watu wengi wanapojisikia kuwa wagonjwa,ununua dawa kwenye maduka hayo na kuanza kuzitumia.

Ni ukweli usiopingika kuwa dawa zimetengenezwa ili kutibu maradhi fulani ambayo yatabainika kwa mgonjwa baada ya uchunguzi wa kitaalamu.

Hivyo, matumizi ya dawa bila kufanya uchunguzi wa kitaalamu yanaweza kuwa na madhara makubwa kwenye afya yako

Yafuatayo ni madhara yatokanayo na kutumia dawa bila ushauri wa daktari:

   Huweza kusababisha kifo
Mosi kama nilivyoeleza kwenye hoja zilizotangulia, dawa ni sumu zinazokabili vimelea vya magonjwa. Hivyo kutumia dawa vibaya kunaweza kusababisha kifo.

Ikumbukwe pia watu wenye matatizo maalumu kama vile maradhi ya moyo pamoja na shinikizo la damu, wanapaswa kuwa makini na dawa wanazozitumia kwani zinaweza kuchochea matatizo yao na hatimaye kifo.

 Huweza kusababisha saratani
Pili dawa zinapoingia mwilini mwako kimakosa na kushindwa kufanya kazi yake, zinaweza kuharibu baadhi ya seli za mwili na kuzifanya kugeuka seli za saratani. Hivyo hakikisha dawa unayoitumia ni sahihi na inalenga ugonjwa husika.

     Husababisha usugu wa maradhi

Tatu, tambua mtaalamu wa afya ukupa kiwango cha dawa kulingana na vipimo alivyovifanya, hivyo kutumia dawa bila vipimo vya kitaalamu kunaweza kusababisha vimelea vya ugonjwa vizoee dawa husika na kusababisha ugonjwa huo usitibike tena.
Hili ndilo linalosababisha maradhi kama vile malaria sugu au UTI sugu. Hivyo kabla ya kutumia dawa ni vyema ukafanya uchunguzi wa kitaalamu.

      Husababisha tatizo la mzio
Nne kuna watu wenye tatizo la mzio au wengi uita aleji, watu hawa wanapaswa kuwa makini na kuepuka kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu.

Hili ni kutokana na baadhi ya dawa kutokuendana na afya zao, hivyo kusababisha tatizo lao la mzio kuibuka. Ni vyema ukamwona mtaalamu wa afya na umweleze aina ya mzio uliyo nayo ili akupe dawa stahiki.

    Huongeza sumu mwilini
Dawa zimetengenezwa kwa kutumia kemikali mbalimbali ambazo kimsingi ni sumu zinazoua vimelea vya magonjwa.

Hivyo kutumia dawa bila vipimo kunakusababishia kuongeza sumu za dawa hizo mwilini mwako kwani umetumia dawa ambazo mwili hauzihitaji kukabili ugonjwa husika.

Sumu hizi zinapokusanyika mwilini mwako zinaweza kukuletea athari mbalimbali za muda mfupi au hata mrefu.

Ni muhimu ukumbuke kuwa dalili za ugonjwa mmoja zinaweza kuwa dalili za ugonjwa mwingine pia. Hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi pamoja na kutafuta ushauri wa kitabibu kabla ya kutumia dawa zozote kutibu maradhi yanayokukabili.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news