Majaliwa awataka Watanzania kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unakuwa wa amani, utulivu

DAR ES SALAAM, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kila Mtanzania anapaswa kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa amani na utulivu. Diramakini inakupa ripoti kamili...endelea,

Majaliwa amesema kuwa kiongozi wa nchi, Rais Dkt.John Pombe Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki.
 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika  Baraza la Eid El Adh’haa  lililofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Ameyasema hayo leo wakati akishiriki swala na baraza la Eid el-Adh’haa iliyofanyika kitaifa  jijini Dar es salaam.

"Ninaamini viongozi wa dini na kila mmoja tunaendelea kuliombea taifa hili ili uchaguzi wa mwaka huu umalizike salama, tujiepushe na lugha za uchochezi, tujiepushe na lugha za bezo, tujiepushe na lugha za kashfa, tuzungumze kile ambacho wananchi hawa utawatendea,"amesisitiza Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema kuwa, kutokana na mfululizo wa matukio ya moto yaliyotokea katika taasisi za dini ya Kiislam ikiwamo Shule za Ilala Islamic na Kinondoni Muslim, Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa dini hiyo wameanza uchunguzi ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.
 
Waumini wa  dini ya Kiislamu wakiswali swala ya  Eid El Adh’haa kitaifa  kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
"Hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria iwapo mtu yoyote atabainika kuhusika na matukio haya ya moto katika taasisi za dini ya Kiislam, kama kulikuwa na dhamira ya mtu binafsi kuharibu miundombinu hii na kutia hasara kwa njama,hatuwezi kumvumilia na kama kutakuwa na makosa ya mifumo tutafuatilia na kufanya marekebisho makubwa," amesema.

Amesema, Rais Dkt. John Magufuli pamoja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wanawatakia watanzania na waislam wote sikukuu njema ya Eid na amepokea salamu za pongezi  zilizotolewa kwa Serikali na viongozi wa dini ya kiislamu namna Serikali inavyosimamia suala la amani nchini.

Pia Waziri Mkuu amewataka Waislam kujiepusha kutoa matamko ya mtu mmoja mmoja yanayoweza kuwavuruga Waislam wote bali waendeleze mshikamano na mahusiano kwa waislam wote na taasisi nyingine.
Waumini wa  dini ya Kiislamu wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati alipokuwa akizungumza katika Swala na Baraza la Eid El Adh’haa kitaifa  kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwa upande wake,Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana amewataka watanzania kutambua kuwa uchaguzi mkuu ni wa watanzania wote, hivyo wanapaswa kuchagua viongozi wanaohitajika na ambao wataweza kukidhi haja za watanzania.

"Hakuna haja ya vurugu, ghasia wala kufanya fujo ya aina yoyote, tushikamane ili kuufanya uchaguzi vizuri, tumalize vizuri na kuijenga nchi yetu kwani sisi sote tunatakiwa tuijenge nchi,"amesema Mufti Mkuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Mwenyenzi Mungu akubariki sana Mzee wetu, Kassim Majaliwa. Hakika umekuwa msaada mkubwa sana kwa jemedari wetu Mheshimiwa Rais Dkt.John Magufuli na Mama Samia katika kuwezesha ustawi wa maendeleo ya Taifa letu. Ishalaah! tutazidi kuwaombea ili muendelee kutuwakilisha Watanzania, maana Mungu amewakirimia kipawa cha kipekee cha utumishi kwa ajili ya kutetea na kulinda maslahi ya Taifa. Endeleeni kuchapa kazi, nasi Watanzania tupo nyuma yenu ili kuhakikisha Tanzania inasonga mbele.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news