Bahrain, UAE zajitenga na Palestina, zaunga mkono Israel

RAIS wa Marekani, Donald Trump ameitangazia Dunia kuwa, Bahrain imejumuika na Umoja wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates) kukubali kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Hayo ameyabainisha baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Al Khalifa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Rais Trump ameitaja Septemba 11, mwaka huu kuwa ya kihistoria na anaamini mataifa mengine yatafuata mkondo huo katika kuimarisha mahusiano hayo na Israel.

Pia kupitia taarifa ya pamoja kati ya Marekani, Bahrain na Israel zimesema kuwa, kufungua mawasiliano ya moja kwa moja na ushirikiano kati ya pande hizo mbili na uchumi ulioimarika utaendelea kuleta mabadiliko ya manufaa katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza uthabiti, usalama na ufanisi katika eneo lote.

Mchambuzi wa masuala ya diplomasia na uhusiano wa Kimataifa ameieleza Diramakini kuwa, hatua hiyo kwa namna moja au nyingine inafaa kupongezwa ingawa kwa upande wa Mamlaka ya Palestina na washirika wake itaonekana ni chungu.

Rais wa Marekani,Donald Trump akifanya mazungumzo na Mfalme wa Bahrain, Hamad bin Isa Al Khalifa, siku ya Jumapili ya Mei 21, 2017 mjini Riyadh. (AP Photo/Evan Vucci/ Diramakini).

"Hatua hii ukiitazama kwa jicho la tatu ni njema sana katika kuimarisha hali ya usalama na uthabiti wa kiuchumi Mashariki ya Kati, hakuna anayependa kushuhudia kila wakati vita, hivyo mpango huu ingawa kwa namna nyingine ni mchungu kwa Wapalestina lakini, unaweza kuwa na tija, ni jambo la kukaa na kutafakari kwa kina kuona ni kwa namna gani wawili hao wanaweza kuridhiana ili amani na mshikamano vitawale,"amesema.

Hatua ya Bahrain na Muungano wa Falme za Kiarabu kuunga mkono Israel inatajwa kuwa huenda itadhoofisha msimamo wa muda mrefu wa mataifa ya Kiarabu unaoitaka Israel kuondoka katika makazi iliyokalia kimabavu na kukubali utaifa wa Palestina kabla ya kurejelea uhusiano wa kawaida na mataifa hayo.

Hivi karibuni Muungano wa Falme za Kiarabu ulikubali kurejesha uhusiano wa kawaida na Israel, chini ya mkataba uliosimamiwa na Marekani unaotarajiwa kutiwa saini katika sherehe itakayoandaliwa katika Ikulu ya White House siku ya Jumanne ijayo.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Muungano wa Falme za Kiarabu, Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahyan wanatarajiwa kuhudhuria katika sherehe hiyo ambapo watatia saini Azimio la Kihistoria la Amani.

Benjamin Netanyahu amesema kuwa, uamuzi wa Bahrain unaadhimisha enzi mpya ya amani kwani kwa miaka mingi wamewekeza katika amani na sasa amani itawekeza kwao na kuleta uwekezaji mkubwa katika uchumi wa Israel.

Aidha, Msemaji wa Kundi la Hamas, Hazem Qassem amesema, uamuzi wa Bahrain wa kurejelea uhusiano wa kawaida na Israel unaashiria madhara makubwa kwa azma ya Palestina.Unaweza kusoma kwa kina hapa.

Kwa upande wake, Hossein Amir-Abdollahian ambaye ni mshauri maalumu wa masuala ya Kimataifa wa Spika wa Bunge la Iran ameutaja uamuzi wa Bahrain kuwa usaliti mkubwa kwa azma ya mataifa hayo ya Kiislamu na Palestina katika Mashariki ya Kati.




Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news