Majaliwa:Chagueni kiongozi atakayelinda amani Tanzania

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wana Tanga na Watanzania kwa ujumla wahakikishe ifikapo Oktoba 28, mwaka huu wanajitokeza kwa wingi kwenda kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kulinda tunu mbalimbali za Taifa ikiwemo amani na Muungano, anaripoti MWANDISHI WETU wa DIRAMAKINI kutoka TANGA.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Tangamano jijini Tanga, Septemba 12, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Ameyasema hayo Septemba 12, 2020 alipokuwa akimuombea kura Rais Dkt.John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini Tanga.

“WanaTanga bila kujali itikadi za vyama nipo hapa mbele yenu kwa unyenyekevu mkubwa nawaomba ifikapo Oktoba 28, mwaka huu tumchague Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ili akaendeleze miradi ya maendeleo aliyoianzisha. Pia nawaomba tumchague Ummy Mwalimu katika nafasi ya ubunge katika jiji letu la Tanga pamoja na wagombea wa udiwani wa CCM,”amesema Waziri Mkuu.

Amesema, wananchi wanatakiwa wamchague Rais Dkt.Magufuli kwa sababu ni kiongozi shupavu mwenye uwezo wa kufanya maamuzi na asiyekubali kuyumbishwa na yeyote.

Wananchi wa Jiji la Tanga wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Tangamano jijini humo, Septemba 12, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Pia Rais Dkt. Magufuli ni kiongozi mwenye kuwajali Watanzania na atakayewaruhusu waendelee kuabudu kwa uhuru na ndio maana hata uchaguzi umepangwa kufanyika siku ya Jumatano ili kutoa fursa kwa wananchi kutumia siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kwa ajili ya kuendelea kuabudu.

Akizungumzia kuhusu miradi ya miundombinu ya barabara inayotekelezwa katika jiji hilo, Mheshimiwa Majaliwa amesema shilingi bilioni 66.8 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Tanga hadi Pangani yenye urefu wa kilomita 50, ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami.

“Shilingi bilioni 2.3 zimetumika kwa ajili ya uwekaji wa taa za barabarani 436 kwa barabara zilizopo ndani ya Jiji la Tanga na taa za kuongoza magari katika barabara ya Mombasa. Ujenzi wa miundombinu hii umeinua uchumi wa wananchi wa Jiji la Tanga kwa kuwawezesha kufanya kazi zao bila vikwazo,”amesema.

Wasanii Mrisho Mpoto (kushoto) na Banana Zoro wakiimba katika mkutano wa kampeni za CCM uliohutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye uwanja wa Tangamano jijini Tanga, Septemba 12, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema, miradi mingine ya kimkakati inayotekelezwa katika jiji hilo ni pamoja na ujenzi wa dampo la kisasa katika eneo la Mpirani Chongoleani ambapo shilingi bilioni 8.9 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa eneo la udhibiti wa taka ngumu na tayari ujenzi umekamilika.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, jumla ya shilingi bilioni 1.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kitega uchumi kwenye stendi ya mabasi ya Jiji la Tanga. Ujenzi unaendelea na upo katika hatua ya umwagaji zege katika ghorofa ya pili.

“Shilingi bilioni 21.9 zimetumika kuboresha miundombinu ya barabara zenye urefu wa kilomita 16.4 kwa kiwango cha lami. Barabara hizo zilizotengenezwa ni barabara ya Sita na barabara ya Chumbageni (km 1), Barabara ya Nne na Chumbageni hadi Ikulu (km 1.14), Barabara ya kutoka Diwani/Ikulu, Taifa na Sahare Phase. I (km 4.2).”

Amesema, barabara nyingine ni barabara ya kutoka Diwani hadi Mwabonde (km 1.62), barabara ya kutoka Mabawa - Msambweni II (km 0.80), barabara ya kutoka Mabawa, barabara ya Nguvumali, barabara ya Nane na Jamatcan (km 3.53), Barabara ya Msambweni na Barabara ya stendi ya Kange (km 5.0).

Mheshimiwa Majaliwa amesema shilingi bilioni 2.2 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa mifereji mikubwa ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 3.44 jijini Tanga. Pia shilingi bilioni 10 zimetumika kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha changarawe na udongo katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza mgombea ubunge wa CCM wa Jimbo la Tanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akiwaomba wananchi wa Tanga wampigie kura Mgombea Urais wa CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Wabunge na Madiwani wa CCM katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Tangamano jijini Tanga, Septemba 12, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



Amesema, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Halmashauri ya Jiji la Tanga imepanga kutumia shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mabawa- Msambweni II na barabara ya 11 na ya 12 kwa kiwango cha lami, ambapo kwa sasa utekelezaji wake upo katika hatua za awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news