TaCRI yawapa tabasamu wakulima wa kahawa Mara, RC Malima aipongeza kwa kuwezesha matokeo chanya

MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) kwa namna ambavyo imeleta matokeo chanya kwa wakulima wa mkoa huo kwa kuwawezesha kuzalisha kwa tija zao la kahawa.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akinywa kahawa alipofika katika banda la TaCRI kutembelea katika ufunguzi wa maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 12 hadi 15 katika viwanja vya Mama Maria Nyerere Butiama Mkoa wa Mara kushoto kwake ni Mtafiti kutoka taasisi hiyo, Jeremiah Magesa. (Picha na Amos Lufungulo/Diramakini).

Ni kwa kuwapa elimu bora, miche bora na kufuatilia kwa karibu wakulima, hatua ambayo imetajwa kuongeza mafanikio na kuendelea kulifanya zao hilo liwe na mchango chanya kwa maendeleo ya uchumi wa wananchi na mkoa kiujumla, anaripoti AMOS LUFUNGULO wa DIRAMAKINI kutoka MARA. 

Malima amesema kuwa, TaCRI imekuwa na mchango mkubwa kwa wakukima wanaolima zao hilo, kwani hapo awali wakulima wengi walitumia miche ambayo haijafanyiwa utafiti na kwamba kanuni bora za kilimo cha zao hilo hazikuzingatiwa kabisa, na hivyo kulifanya zao la kahawa kushindwa kuwa na mchango wa kiuchumi kwa wananchi, lakini kwa sasa amesema linapaswa kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati yatakayokuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na pato la mkoa.

Malima ameyasema hayo Septemba 12, mwaka huu akiwa katika banda la TaCRI alipotembelea na kujionea uzalishaji wa miche bora ya kahawa katika ufunguzi wa maonesho ya nane nane yanayoendelea kufanyika viwanja vya Mama Maria Nyerere Butiama Mkoa wa Mara kuanzia Septemba 12 hadi 15 ambayo yanaambatana na maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day) ambayo hufanyika kila mwaka mwezi Septemba ambapo nyumbu kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti huvuka mto Mara kwenda Masai Mara nchini Kenya na kitendo hicho huwa fursa kwa shughuli za utalii.

"Natoa pongezi nyingi za dhati kwa TaCRI mmesaidia kwa kiwango kikubwa sana kuinua zao la kahawa katika Mkoa wa Mara ingawa bado hatujafikia malengo kisawasawa, kahawa ya Mkoa wa Mara ni kahawa bora kabisa nimeiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuweka fedha nyingi zisaidie katika uoteshaji wa miche na kusaidia shughuli za utafiti ili TaCRI wazidi kutusaidia kama wanavyofanya.

Pichani Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima kushoto akipewa ufafanuzi na Meneja wa TaCRI Kanda kituo kidogo cha Sirari, Almas Hamad alipofika katika banda la taasisi hiyo kujionea miche ya kahawa inavyooteshwa na kutunzwa katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwa siku nne katika viwanja vya Mama Maria Nyerere Butiama Mkoa wa Mara.(Picha na Amos Lufungulo/ Diramakini).

"Pia tuitangaze kahawa yetu ya Mkoa wa Mara kwa sababu kahawa yetu ni miongoni mwa kahawa bora sana ya Arabika Afrika inayozalishwa cha msingi tuzidi kuitangaza iwe kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika mkoa wetu,"amesema Malima.

Kwa upande wake Jeremiah Magesa ambaye ni Mtafiti kutoka TaCRI amesema kuwa,kahawa inayozalishwa Mkoa wa Mara ni kahawa yenye ubora wa hali ya juu, ambapo amewahimiza wananchi mkoani Mara kuendelea kulima zao hilo kwa kupanua uzalishaji kwa tija, hasa kwa kuzingatia kanuni bora wanazohimizwa kuzingatia ili iwaletee maendeleo na kuwakwamua kiuchumi.

Naye Meneja wa TaCRI Kanda, Kituo kidogo cha Sirari, Almas Hamad amesema kuwa ili kuzalisha kwa tija wakulima wa kahawa lazima wapate miche bora na kuzingatia kanuni bora kuanzia upandaji hadi uvunaji ikiwemo kupandia mbolea, kuzingatia ubora wa shamba, kutunza miche na kwamba hatua ya uvunaji lazime ifanywe kwa ubora uanikaji baada ya kuvunwa hadi hatua ya ukoboaji.

Pichani Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliyeshikilia mche wa kahawa akipokea maelezo kutoka kwa Meneja Kanda kituo kidogo cha Sirari, Almas Hamad alipofika katika banda hilo kujionea namna ambavyo miche hiyo huoteshwa na kutunzwa. (Picha na Amos Lufungulo/Diramakini).

Meneja Hamad ameongeza kuwa katika kuhakikisha kahawa inalimwa kwa wingi katika Mkoa wa Mara, halmashauri zinazolima kahawa zinapaswa kuwa na vitalu vya kuzalisha miche ya kahawa, TaCRI iweze kupewa fedha nyingi za kuzalisha miche bora ambapo mche mmoja utaweza kuzalisha kuanzia kilo tatu na kuendelea, huku akibainisha kuwa hekari moja inaweza kupandwa miche 867 ikichanganywa na migomba 133 kwa nafasi ya mita mbili kwa mbili ya kahawa, mkulima atapata kahawa kwa wingi na atauza kwa fedha nzuri na atajipatia maendeleo kutokana na zao hilo.

Petro Mwita (Nyeusi) mkulima wa kahawa kutoka Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara ameieleza Diramakini kwamba, tangu alipoanza kutumia miche bora ya kahawa na kuzingatia elimu ambayo imekuwa ikitolewa na TaCRI juu ya uzalishaji wa kahawa kwa tija ameweza kuondokana na umaskini.

Mkulima huyo amesema,tayari amejenga nyumba bora ya kuishi, kusomesha watoto wake ambapo kwa sasa amesema maisha yake yamebadilika tofauti na awali alipokuwa akipanda miche ya kahawa ya zamani.

"Tangu TaCRI walipoleta mbegu hizi chotara za kahawa, uzalishaji wangu umeongezeka sana na hata kahawa nayovuna ina ubora mkubwa mathalani, nimeongeza kipato kutoka dola 65 hadi dola 120 wakati mwingine zaidi ya hapo hadi 140 kwa gunia, ambapo kwa msimu napata gunia 37- 40 ama zaidi na misimu huwa ni miwili mkubwa na mdogo kiukweli kahawa imenikomboa na pia namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima kwa mikakati yake thabiti kututengenezea mazingira bora sisi wakulima wa kahawa na mazao mengine ndani ya mkoa wetu,"amesema Mwita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news