Mgombea Urais Bernard Membe afunguka

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Bernard Membe amesema kuwa, hali ya kusuasua kwa kampeni hususani kwa vyama vya upinzani nchini kumechangiwa na ukata.

Amesema, wagombea wengi kwa sasa wanakabiliwa na ukata mkubwa wa kifedha tofauti na chaguzi zilizopita, hivyo ni vigumu kusonga mbele kwao.

Mgombea Urais huyo ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuwasili leo Septemba 15, 2020 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) uliopo jijini Dar es Salaam kutokea Dubai, Falme za Kiarabu.

Amesema, kwa sasa wamekosa mbio kwa sababu wadau wengi ambao walikuwa msaada kwao awali na wanaokubalika kisheria wamekimbia.

"Hatuna fedha, maana wafanyabiashara wote wanaotoa fedha wamekimbia ni wale ambao wanakubalika kisheria kwa ajili ya kuunga mkono hatua hizi, hivyo vyama vyenye wagombea vinaukata wa fedha, havina uwezo wa kufanya kampeni, maana hata timu za kampeni hawana,"amesema.

Akizungumzia kuhusiana na safari yake ya kwenda Dubai, Membe amesema kuwa, hiyo ni sehemu ya ratiba yake ambayo huwa anafanya hivyo kila mwaka kwa kuwa, huko kuna kampuni ambayo yenye pia ni mwanachama.

Pia amesema,huwa anaenda Dubai mara nne kwa mwaka, na hakwenda mara mbili, hivyo sasa aliamua kwenda huko ikiwemo kuangalia afya yake.

Mbali na hayo amesema, kwa sasa wanakabiliwa na kikwazo kingine cha kuingiza au kutoa fedha nje ya nchi, jambo ambalo pia linachangia ugumu katika kampeni zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news