TAKUKURU yavuruga dili la wapigaji, mtego waondoka na watu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rusha (TAKUKURU) katika mikoa ya Manyara na Tanga imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuendelea kuhakikisha vitendo vya kutoa na kupokea rushwa nchini vinatokomezwa kabisa ili kuwezesha jamii na Taifa kusonga mbele kiuchumi.

Manyara

Katika Mkoa wa Manyara TAKUKURU inamshikilia Ruth Reniel Semkuyu ambaye ni mtumishi wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Babati kwa makosa ya kudai na kupokea rushwa ya shilingi laki moja kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Makungu kupitia taarifa iliyoonwa na www.diramakini.co.tz amebainisha kuwa, "awali tulipokea taarifa kutoka kwa mlalamikaji (jina linahifadhiwa) ambaye alishinda kesi yake katika moja ya mabaraza ya kata Mkoani Manyara, hivyo alikuja Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Babati ili kukaza hukumu.

"Alipofika kwenye baraza hilo, alielekezwa amuone Ruth Semkuyu ili ampe utaratibu wa kukaza hukumu, na alipokutana na Ruth, Ruth alimtaka kupeleka jumla ya shilingi laki moja na elfu kumi na nane tu kwa madai kuwa hiyo ndiyo gharama ya kukaza hukumu. Mwananchi huyo alitilia mashaka kiwango hicho cha fedha na hivyo akaamua kuleta malalamiko TAKUKURU.

"Uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Manyara ulibaini kuwa fedha halali zilizokuwa zinatakiwa kulipwa kama gharama ya ukazaji hukumu ni shilingi 18, 000, hivyo tuliandaa mtego wa jumla ya shilingi 118, 000."Ruth alipokea fedha hizo akiwa ofini kwake, kisha akaandaa control number na akamrejeshea mlalamikaji wetu  shilingi 18,000 na kumuelekeza akalipe kiasi hicho cha sh.18,000 katika benki kisha alete risiti.

"Baada ya hatua hiyo, Ruth alikamatwa na makachero wetu akiwa na rushwa ya shilingi 100, 000 ambayo alishindwa kujieleza fedha hiyo ni ya nini. TAKUKURU Mkoa wa Manyara inaendelea kumshikilia Ruth na mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote mara uchunguzi utakapokamilika.

"Ni rai yetu kwa watumishi wa umma mkoani Manyara kuridhika na vipato wanavyopewa na mwajiri wao. Tuwaombe pia wananchi waendelee kutoa taarifa kwa ofisi za TAKUKURU zilizoko karibu nao au kwa namba yetu ya dharura 113 ambayo mwananchi hapaswi kulipa ili tuweze kuwaondoa watumishi wachache ambao bado hawaridhiki na kipato halali wanacholipwa na mwajiri,"amefafanua Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Makungu.

Tanga

Wakati huo huo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga imefanikiwa kuokoa na kurejesha fedha shilingi milioni 16,585,443.00 za SACCOS ya Umoja wa Vijana Pangani na Mwalimu mstaafu.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Dkt.Sharifa Bungala kupitia taarifa iliyoonwa na www,diramakini.co.tz "Awali ya yote tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha tena nanyi hapa katika Wilaya ya Pangani ambapo leo tutakuwa na tukio la kukabidhi fedha zilizookolewa kutokana na jitihada za TAKUKURU za kuwaondolea kero wananchi wa mkoa wa Tanga.

"TAKUKURU Mkoa wa Tanga tunapenda kutoa taarifa kuhusu kuokolewa kwa fedha kiasi cha shilingi 16,585,443.00 katika Wilaya ya Pangani ambazo leo hii tarehe 09/09/2020 zitakabidhiwa kwa wahusika kama ifuatavyo:

"Wa kwanza ni SACCOS ya UMOJA WA VIJANA PANGANI (UVIPASA) ambayo itakabidhiwa Shilingi 12,185,443 na Mhusika wa pili ni mwalimu mstaafu, HATIBU FUE MKANZA ambae tutamkabidhi Shilingi 4,400,000 zilizotokana na mikopo umiza.

FEDHA ZA UVIPASA SHILINGI 12,185,443

"TAKUKURU Wilaya ya Pangani imeokoa jumla ya shilingi 12,185,443 kati ya shilingi 13,000,000 kutoka kwenye uongozi wa zamani wa SACCOS ya UMOJA WA VIJANA PANGANI (UVIPASA) zilizokuwa zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mwaka 2013 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kukopa ili kuinua mitaji ya biashara zao na baadaye kuzirudisha kwa mujibu wa mikataba yao.

"Lakini viongozi hao hawakurejesha fedha hizo kwa zaidi ya takribani miaka sita (kutoka mwaka 2014 hadi mwaka 2020 uchunguzi huu ulipoanzishwa) na kulazimika kuzirejesha fedha hizo baada ya TAKUKURU wilaya ya Pangani  kuingilia kati dhuluma hii.

"Operesheni hii imefanyika kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa TAKUKURU mkoa wa Tanga na baadhi ya  wanachama wa SACCOS wakiwalalamikia baadhi ya wanachama na viongozi wa umoja huo kuchukua mikopo kwenye chama hicho tangu Mwaka 2014 na kukaidi kurejesha kwa zaidi ya miaka 6 hali amabayo iliifanya SACCOS hiyo kushindwa kujiendesha ikiwemo kutorejesha akiba za wananchama wanaojitoa au wanaopunguza hisa zao.

"Pamoja na kukabidhi fedha hizi TAKUKURU Wilaya ya Pangani bado inaendelea kuwatafuta viongozi na

wanachama wa Saccos hii ambao bado wanadaiwa na hakika mkono wa Serikali utawafikia. Tunatoa agizo kwa wale wote wanaodaiwa kujisalimisha na kurejesha fedha hizo katika Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Pangani kabla ya sisi kuwafikia,"amebainisha Kaimu Mkuu huyo wa TAKUKURU.

FEDHA ZA MWALIMU HATIBU FUE MKANZA SHILINGI 4,400,000

"Mnamo terehe 05/05/2020 ofisi ya TAKUKURU (W) Pangani ilipokea malalamiko toka kwa mwalimu mstaafu  HATIBU FUE MKANZA akimlalamikia mkopeshaji binafsi ndugu MABOGA JUMA HITIRA kuwa mnamo mwaka  2017 alimkopesha fedha kiasi cha shilingi 4,000,000 kwa makubaliano kuwa atamrejeshea fedha hizo baada ya kulipwa mafao yake ya kustaafu na kwamba katika makubaliano yao riba ya mkopo haikuwekwa bayana kwa mkopaji.  

"Ilidaiwa katika taarifa ya malalamiko kwamba mafao ya mstaafu huyo yalipotoka tarehe 11/10/2018 mkopeshaji huyo alimtaka amlipe jumla ya Shilingi 16,000,000 fedha ambayo ni Shilingi 12,000,000 (milioni kumi na mbili) zaidi ya kile alichopokea kutoka kwa mkopeshaji.

"Ilidaiwa na mlalamikaji kwamba kutokana na mazingira yaliyokuwepo na jinsi mkopeshaji alivyombana hadi kufikia tarehe ya kuwasilisha malalamiko yake TAKUKURU tayari mkopeshaji alikwishakuchukua toka kwake jumla ya shilingi 9,430,000 fedha ambazo alimlipa kupitia mafao yake ya kustaafu na kupitia pension yake ya kila mwezi.

"Taarifa ilieleza kwamba pamoja na mkopeshaji huyo kuchukua fedha yote hiyo bado anaendelea kumhujumu kwa kumtaka aendelee kumlipa hadi ifikie 16,000,000 bila ya uhalali wowote.

"Baada ya mtoa taarifa kubaini kuwa alidhulumiwa na mkopeshaji huyo na kwamba baada ya kuona na kusikia kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwamba baadhi ya wastaafu wamekuwa wakirejeshewa fedha zao kwa msaada wa TAKUKURU, naye aliamua kufika TAKUKURU wilaya ya Pangani ili aweze kupata haki yake.

"Baada ya TAKUKURU wilaya ya Pangani kupokea malalamiko hayo uchunguzi ulifanyika ili kubaini uhalali wa mtuhumiwa kujipatia fedha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni nane toka kwa mlalamikaji na huku akidai aendelee kulipwa hadi ifike shilingi 16,000,000. Baada ya uchunguzi yafuatayo yalibainika:

"Kwamba ni kweli mlalamikaji alichukua kiasi kisichozidi milioni nne toka kwa mkopeshaji na ni kweli kuwa  amemlipa mkopeshaji huyo jumla ya shilingi 8,400,000 kati ya shilingi 16,000,000 anazotakiwa kumlipa mkopeshaji.

"Kwamba mkopeshaji huyo ni mdanganyifu kwani anafanya biashara ya ukopeshaji fedha bila ya kufuata sheria za nchi ikiwemo ya kupata vibali vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kulipa kodi kutokana na faida anayozalisha.

"Kwamba mkopeshaji alimlaghai mlalamikaji kwa kumsainisha mikataba ya udanganyifu na yenye dhuluma kwani katika mikataba alimjazisha kiasi tofauti na alichompatia kwa lengo la kuficha riba halisi ili aweze kuhalalisha malipo ya shilingi milioni 16.

"Kwamba baada ya mahesabu kufanyika ilibainika kuwa riba ya mkopo huo ni asilimia 300 (%) ya fedha aliyokopeshwa mlalamikaji. Baada ya mlalamikiwa kuhojiwa alikiri kuwa ni kweli alimkopesha fedha mlalamikaji. lakini ni fedha ambayo haizidi shilingi 4,500,000 lakini katika mikataba alikuwa anamsainisha kiwango kikubwa kuliko alichompatia akiimanisha kuwa ni riba ya mkopo.

Aidha alikiri kuwa pamoja na kuwa alidai kuwa anakopesha fedha lakini hakuwa na uhalali wowote wa kufanya biashara hiyo.

"Kutokana na ushahidi uliopatikana TAKUKURU mkoa wa Tanga ilimuamuru mtuhumiwa MABOGA JUMA HITIRA kumrejeshea mlalamikaji Shilingi 4,400,000 na kusitisha madai na makato yote aliyokuwa anafanya dhidi ya mlalamikaji kwa lengo la kutaka alipwe hadi shilingi 16,000,000.

"TAKUKURU mkoa wa Tanga inawasihi viongozi wa SACCOS kutoka ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na SACCOS yenyewe kusimamia marejesho ya mikopo itakayotolewa kutokana na fedha hizi ambazo leo TAKUKURU Wilaya ya Pangani inawakabidhi, kwa umakini na uaminifu, kwa lengo la kuhakikisha kwamba walengwa wa SACCOS hii wananufaika na nia njema ya Serikali ya kuinua uchumi wa wananchi wake katika Wilaya ya Pangani na hatimaye nchi nzima.

"Aidha tunawasihi wafanyabiashara wote wa mkoa wa Tanga kufanya biashara kwa mujibu wa sheria za nchi kwani kinyume na hapo TAKUKURU mkoa wa Tanga haitasita kuwachukulia hatua za kisheria," amefafanua Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Dkt.Sharifa Bungala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news