Tanzania ipo salama, usituchokoze, kuwa mzalendo-Polisi

Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma, SACP David A. Misime.

JESHI la Polisi nchini limetoa onyo kwa mtu au kikundi chochote ambacho kitafanya fujo wakati huu wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma, SACP David A.Misime kupitia taarifa iliyoonwa na www.diramakini.co.tz hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari na hawatarajii kushuhudia yeyote ambaye atakwenda kinyume.

"Kwanza niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuhabarisha na kuelimisha wananchi juu ya masuala mbalimbali yakiwemo ya kiusalama hususani katika kuwawezesha kutambua umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu na wahalifu.

"Lakini kubwa zaidi ni suala la kuelimishana kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kulinda amani, usalama na utulivu wa nchi yetu Tanzania.

Ndugu waandishi wa habari,jambo la pili, napenda kuwajulisha kuwa hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari na   tunaendelea vizuri na usimamizi wa ulinzi katika kampeni zinazoendelea katika maeneo mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, 2020 kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, wananchi na wadau wengine.

"Aidha, napenda kuwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi limejiandaa vizuri kukabiliana na matishio ya aina yeyote ya kiusalama, hata hivyo, hadi sasa hakuna matishio makubwa ya kiusalama, kwani ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya nchi ili kuhakikisha kampeni zote na Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa amani na utulivu.

"Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi, viongozi kisiasa na wadau wengine wote wa uchaguzi kuendelea kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria za nchi zinavyoelekeza kwa kutambua kuwa hakuna haki yoyote iliyotolewa na sheria mama (Katiba) na sheria nyingine za nchi isiyokuwa na wajibu ikiwa ni pamoja na kutenda  haki, kuepuka mihemko itakayokusukuma kujichukulia sheria mikononi, kutokutoa maneno ya uchochezi na uchonganishi, kutoa  maneno ya kuhamasisha chuki, kukashifu wengine, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa kusambaza uzushi na mambo ya uongo na mengine mengi yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani, usalama na utulivu wa nchi yetu.

"Napenda kuwajulisha kuwa pamoja na ushwari huo unaoendelea katika kampeni zinazoendelea yapo matukio machache yaliyopangwa na kutekelezwa na watu wachache wasioitakia mema nchi yetu.   

"Kwa mfano kule jijini Arusha kulitokea tukio la kuchoma moto ofisi, mkoani  Kilimanjaro kulitokea tukio la  kurushia mawe msafara, Songwe kulifanyika mauaji na kujeruhi, Mbeya kuchoma nyaraka na vifaa vya ofisi moto.
"Hata hivyo kutokana na jitihada za Jeshi la Polisi na ushirikiano wa wananchi wema,watuhumiwa waliopanga na   kufanya uhalifu huo wameshakamatwa na kufikishwa mahakamani.

"Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutii sheria za nchi bila shuruti, kwani kwa kutofanya hivyo kutawaingiza katika matatizo ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani na kupoteza muda wao muhimu wa kujiletea maendeleo, kuiacha familia kama walivyofanya baadhi ya waliokimbia ambao bado wanaendelea kutafutwa na polisi. Pia, tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kuwaepuka na kutofuata kauli za wale wanaojaribu kila mara kutaka kuvuruga amani, usalama na utulivu wa nchi yetu,"amefafanua Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma, SACP David A. Misime.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news