Vedastus Mathayo anadi Ilani kisayansi Musoma Mjini,wafuasi CHADEMA,CUF waunga mkono

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini Kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Vedastus Mathayo ameendelea na kampeni siku ya pili ya kuomba kura kwa wananchi kuwania ubunge wa jimbo hilo katika Kata ya Rwamulimi.
Amesema, endapo akichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, atatatua tatizo la ubovu wa barabara ziweze kupitika katika kata hiyo kufuatia kuathiriwa na mvua pamoja na madaraja ili mtandao wa mawasiliano uweze kuimarika, anaripoti AMOS LUFUNGULO kutoka MARA.

Mbali na hilo, Mathayo amesema endapo akishinda ndani ya kipindi cha miaka mitano atahakikisha anashirikiana na wananchi na Serikali kujenga kituo cha afya ili kusogeza huduma za afya kwa karibu na wananchi wa kata hiyo, sambamba na kuimarisha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa kata hiyo ya Rwamulimi.

"Hivi ninavyozungumza Kiwanda Cha MUTEX pia kimepata mwekezaji na mazungumzo yapo katika hatua nzuri na Serikali, kiwanda hiki kitaanza kufanya kazi ili vijana ambao hawana kazi wapate ajira kwa ajili ya kujipatia fedha ambazo zitasaidia kuendesha maisha yao, binafsi na kuongeza mzunguko wa kiuchumi katika manispaa yetu ya Musoma cha msingi mzidi kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa kukichagua katika uchaguzi wa mwaka huu,"amesema Mathayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini,Benedictor Magiri amesema Serikali imeutendea haki Mkoa wa Mara kwa miaka mitano iliyopita kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo ikiwemo za ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kwangwa Musoma, kubooresha Shule ya Msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere , utekelezaji wa ujenzi vituo vya afya, Zahanati pamoja na miradi ya maji.
Vedastus Mathayo Mgombea Ubunge Musoma Mjini akiomba kura kwenye Mkutano ukiofanyika Rwamulimi musoma.(Picha na Amos Lufungulo).

Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini Hasan Milanga amesema,hadi sasa kata 47 kati ya kata 178 za Mkoa wa Mara Chama Cha Mapinduzi kimepita bila kupingwa pamoja na Jimbo la Butiama huku akibainisha kuwa, CCM ndiyo chama pekee kilichosimamia amani iliyopo nchini na utengamano wa Kitaifa pamoja na kukomboa baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Angola, hivyo eananchi waendelee kukiamini kuongoza nchi.

Ameongeza kuwa, CCM ndiyo chama thabiti chenye kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania kutokana na misingi yake imara ya chama hicho pamoja na ilani yake ambayo imesheheni mambo muhimu ya kuwafanyia Watanzania hasa kuendelea na ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo, ujenzi wa miradi ya jamii, miundombinu kwa maslahi mapana ya wananchi wote.

Naye Mgombea Udiwani wa Kata ya Makoko ambaye pia ni meya wa Manispaa ya Musoma anayemaliza muda wake, Wiliam Gumbo amesema katika kipindi cha miaka mitano alisimamia ujenzi wa barabara za lami kupitia fedha zilizotolewa na Rais Magufuli katika Manispaa ya Musoma ujenzi wa zahanati, mafanikio ambayo yamechagizwa na uchapakazi wa Mbunge huyo kuiomba serikali itekeleze mradi huo katika kipindi cha miaka mitano.

Fabian James na Elizabeth Yungishi ni wananchi wa Kata ya Rwamulimi wakizungumza na Diramakini baada ya mkutano huo, wamesema watafurahi endapo Mathayo akishinda na kushughulikia kwa haraka uimarishaji wa barabara za kata hiyo ili kuwaondolea adha wananchi pamoja na ujenzi wa Kituo cha afya Kama alivyoahidi.

Katika mkutano huo, wanachama wawili kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mmoja Chama cha Wananchi (CUF) wamejiunga na CCM kutokana na sera bora na maendeleo yaliyotekelezwa na Chama Cha Mapinduzi chini ya Rais John Magufuli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news