Wajane, Masheikh, walimu waahidi kura za kishindo kwa Dkt.Hussein Mwinyi, naye awaahidi neema tele

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo atapata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar, atasimamia haki za wajane kwa kutunga sheria za kulinda maslahi yao, anaripoti Mwandishi Diramakini (Pemba).

Amesema, sheria hiyo itakuwa na nafasi ya kuwabana baadhi ya wanaume wanaotelekeza watoto pindi tu wanapowaacha wanawake.

Amesema, anaelewa changamoto kadhaa zinazowakumba wanawake hao, iwe kwa wale wanaoachwa au kufiwa na waume, kwa kukoseshwa haki zao na kutupiwa mzigo wa malezi na huduma kwa watoto.

Mgombea huyo wa urais ameyasema hayo Septemba 30,2020 katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi mjini Wete Pemba, alipokuwa akizungumza na wanachama wa Jumuiya ya Wajane Zanzibar kwa upande wa Pemba.

“Mungu akinijaliwa kuwa Rais wa Zanzibar nitatunga sheria kali za kuwawezesha wajane kupata haki zao kama yalivyo makundi mengine,pia nitakuwa mstari wa mbele kuhakikisha mateso na udhalilishaji dhidi yenu vinathibitiwa,"amesema Dkt.Mwinyi.

Amesema, anatambua kuwa Zanzibar lipo kundi kubwa la wajane ambalo linaendelea kuteseka na kuhangaika huku na kule na wale wanaume waliowaacha, wakishindwa kuwapata huduma.

Amesema, kwa vile wameshaanzisha umoja wao, kwake itakuwa rahisi kulisaidia kundi hilo ni pale atakapopata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar.

Alieleza, yapo maeneo matatu makubwa ambayo wajane hao wanapaswa kusaidia, ambapo moja wapo ni kupata haki zao kisheria kwa haraka.

“Nikiingia madarakani tu, nitaangalia uwezekano mkubwa, ili wajane wawe wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria, maana haiwezekani kuachwa kwako au kufiwa na muume, iwe ndio waishi kwenye mazingira magumu,’’ameeleza.

Eneo jingine alililotaja mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kuwa atalishughulikia kama akipewa ridhaa, ni kuwawezesha kiuchumi kupitia jumuiya yao.

“Tukiwawezesha kiuchumi wajane wa Zanzibar, itasaidia sana kwa wale ambao pia wana watoto kupata mtaji wa kuwahudumia, ili waishi kwa amani,’’amefafanua.

Hata hivyo amesema hayo yote yanawezekana, ikiwa pia watakiunga mkono Chama Cha Mapinduzi, kuelekea uchaguzi mkuu wa vyama vingi mwezi Oktoba, mwaka huu.

Katika hatua nyingine Dkt.Mwinyi amekubali ombi la jumuiya hiyo kuwa, kama akipata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar, mke wake Maryam Mwinyi awe mlezi wa jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wajane Zanzibar, Tabia Makame amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji.

“Tumekuwa kama vile hatuna thamani mbele ya jamii, kwa sababu ya ujane wetu, sasa mgombea urais, tunaomba kama ukitapata ridhaa, utunyamazishe kilio chetu,’’alieleza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa jumuiya hiyo, Mgeni Hassan Juma amesema wajane wa Zanzibar wamejenga matumaini makubwa na Dkt.Mwinyi.

Mapema Dkt.Mwinyi alikutana na masheikh na walimu wa wilaya hiyo na kuwahakikisha kuwa kama akipata ridhaa ya kuwa rais, ataandaa mpango maalum, ili kuimarisha usomeshaji wa Qur-ani Tukufu.

“Ni kweli kwa sasa mfumo ulivyo, watoto wetu wanaelekea mno kwenye elimu ya skuli na muda mdogo ndio unawakuta madrassa hilo sio sahihi, lazima tuandae mifumo ambayo itawapa watoto fursa ya kusoma maeneo yote,’’ameeleza.

Aidha mgombea huyo, alisema anakusudia kuona anaziimarisha madrassa za kur-an, kuwapatia vitendea kazi waalimu, mishahara ili wafanye kazi kwa kujiamiani.

“Haiwezekani, waalimu wetu wanaotusomesha elimu itakayotufaa akhera wawe duni, na wengine waendelee kupokea mishahara, lazima na wao tuwawekee utaratibu wa kunufaika,’’alifafanua.

Hata hivyo, aliwaahidi viongozi hao wa dini kuwa akipata ridhaa atarejesh mfumo wa zamani wa kuwapeleke masomoni viongozi wa dini, katika nchi mbali mbali.

“Nakiri kuwa utaratibu wa masheikh na vijana wetu kuwapelekea nje ya nchi kwenda kuongeza elimu ni mzuri, na mimi hili litalifanya,’’alisema.

Mmoja kati ya masheikh hao, Sheikh Mohamed Ismail, alisema kinachowakereketa ni kuona masheikh wenzao hawafikishwi mahakamani na wanaendelea kushikiliwa rumande huko Tanzania bara kwa muda mrefu.

Nae Sheikh Mohamed Fumu, alisema kutokana na dhamira yake njema mgombea huyo wa nafasi ya urais wa tiketi ya CCM, watamuunga mkono kwa kumpa kura Oktoba 28, mwaka huu.

“Kwa hakika nyota njema huonekana mapema, maana hili la kukutana na sisi, sio jambo dogo, katika umri wangu huu ni mara ya kwanza, kuitwa na mgombea,’’alieleza.

Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika ziara yake ya kukutana na makundi mbalimbali, alianza na wakulima wa zao la karafuu, viungo, chumvi, wajane, viongozi wa madhebu ya dini, wavuvi na mafundi wa gereji visiwani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news